HabariSiasa

Sababu ya kesi dhidi ya Jaji Mwilu kusitishwa

August 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

RICHARD MUNGUTI na PETER MBURU

MAHAKAMA Kuu Jumatano imesitisha kusikizwa kwa kesi dhidi ya Naibu Jaji Mkuu (DCJ) Bi Philomena Mwilu huku jaji Enock Chacha Mwita akisema haki za Bi Mwilu zimekiukwa na sharti apewe muda awasilishe ushahidi.

Wakili Okong’o Omogeni alimweleza Jaji Mwita kuwa DCJ alisomewa mashtaka ambayo hayana msingi kisheria.

Bw Omogeni alisema kukubalia kushtakiwa kwa Bi Mwilu ni kuhujumu uhuru wa idara ya mahakama.

Jaji Chacha Mwita alisema kuna masuala ya kikatiba ambayo yanafaa kuangaziwa katika kesi hiyo, kwa misingi kuwa ni suala la kibiashara na hivyo kuibua maswali ikiwa linaweza kufanya jaji kukamatwa.

Naibu Jaji Mkuu (DCJ) Bi Philomena Mwilu akiwa mahakamni wakati wa kusikizwa kwa kesi dhidi yake Agosti 29, 2018. Picha/ Richard Munguti

Alielekeza Bi Mwilu pamoja na wakili Stanley Kiima kufika mbele ya mahakama kuu Oktoba 9 ili masuala hayo yaamuliwe.

Hatua hiyo ya Jaji Mwita imekuja baada ya wakili wa Bi Mwilu, Seneta James Orengo kuibua hoja kuwa kesi inayomkumba mteja wake si ya jinai, na hivyo kuiwajibisha mahakama kuamua ikiwa Jaji Mwilu alifaa kukamatwa.

“Ni jukumu la korti kuamua kuwa kesi hii ni ya kijamii na wala si ya jinai, wala haiwezi kuwachia jukumu hilo mawakili wa mshtakiwa wala idara za DPP na DCI,” Bw Orengo akaeleza korti Jumatano.

Mahakama ilielezwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Noordin Haji alikosea kumfungulia mashtaka DCJ Mwilu.

Jaji Mwita alielezwa hakimu mwandamizi Lawrence Mugambi hana mamlaka ya kusikiza kesi dhidi ya DCJ.

Jaji Mwita alisema masuala ya kisheria anayozua DCJ Mwilu na wakili Stanley Kiima ni mazito na yanahitaji kujadiliwa na uamuzi kutolewa.