Habari

SAKATA YA RIO: Wario asimamishwa kazi ya ubalozi

October 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

WAZIRI wa zamani wa Michezo aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Austria Bw Hassan Wario sasa amesimamishwa kazi kufuatia kushtakiwa kwake kuhusiana na kashfa ya michezo ya Olimpiki ya 2016 ambapo serikali ilipoteza zaidi ya Sh55 milioni.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji kupitia kwa naibu wake Bi Emily Kamau aliambia mahakama inayoamua kesi za ufisadi (ACC) kuwa mtumishi wa umma yeyote anayeshtakiwa husimamishwa kazi mara moja hadi uamuzi utolewe.

“Bw Wario hawezi kuendelea na kazi yake ya ubalozi kwa vile amesimamishwa kazi,” Bi Kamau alimweleza hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti.

Akisoma Kifungu nambari 62 cha sheria za hujuma za kiuchumi na ufisadi, Bi Kamau alisema kwa mujibu wa kifungu hicho kuwa Bw Wario hataendelea kutekeleza majukumu yake kama balozi hadi mahakama itakapoamua hatima yake.

Bw Wario asema na jamaa zake alipokuwa akisubiri kuitwa kizimbani Oktoba 19, 2018. Picha/ Richard Munguti

Kiongozi huyo wa mashtaka alieleza DPP atawasiliana na afisi inayoteua mabalozi kisha apate barua atakayowasilisha mahakamani Novemba 16, 2018 ikieleza hatua kamili iliyochukuliwa dhidi ya Bw Wario.

Aidha, naibu DPP alisema serikali itamteua balozi mwingine na familia ya mshtakiwa itarudishwa nchini.

Bi Kamau alieleza msimamo wa serikali baada ya wakili wa Bw Wario, Bw Riogers Sagana kuomba balozi huyo arudishiwe pasipoti yake arudi kazini nchini Austria alikoteuliwa kuwa balozi mapema mwaka huu.

Bw Sagana alianza kwa kueleza mahakama alimsalimisha Bw Wario kwa mkurugenzi wa uchunguzi jinai (DCI) Alhamisi kama ilivyoagizwa na mahakama Jumanne.

Kutoka Kulia: Waziri wa zamani wa Michezo Hassan Wario, Harun Komen Chebet na Patrick Kimathi Nzambu wakiwa kizimbani. Picha/ Richard Munguti

Alisema mshtakiwa alirejea nchini kutoka Austria ambapo familia yake inaishi.

“Naomba hii mahakama imrudishie Bw Wario pasipoti yake. Tayari amenunua tikiti ya ndege kurudi anakohudumu kama balozi,” alisema Bw Sagana.

Wakili huyo alisema Bw Wario aliyeshtakiwa Ijumaa kwa kufuja pesa za umma Sh5.8 milioni kwa kuwapa watu ambao hawakuwa wanariadha kwenda hadi mjini Rio De Janeiro nchini Brazil 2016, atarudi tena nchini wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo mnamo Novemba 16, 2018.

“Mshtakiwa atarudi tena wakati wa kutajwa kwa kesi inayomkabili Novemba 16. Naomba arudishiwe pasi aweze kusafiri,” alirai Bw Sagana.

Wanahabari wa humu nchini na kimataifa walimiminika kortini huku Naibu DPP Bi Emily Kamau alipoitaka korti impe muda Kipchoge Keino akamilishe mahojiano na idara ya upelelezi DCI. Picha/ Richard Munguti

Mahakama ilielezwa mshtakiwa ameahidi kutii masharti atakayopewa na korti.

Lakini mahakama ilielezwa suala la ajira ya Bw Wario limekumbwa na utata na kizungumkuti kwa vile baada ya kushtakiwa hapasi kuhudumu wadhifa wowote wa umma hadi mahakama imwondolee lawama.

Bw Ogoti alimwamuru Bw Wario awache pasipoti yake kortini kama sharti moja la kuachiliwa kwa dhamana katika kesi aliyokana ya kufuja pesa za umma.

Bw Wario alishtakiwa pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa masuala ya michezo Bw Haron Komen Chebet na  meneja wa fedha Bw Patrick Kimathi Nzabu.

Waziri huyo wa zamani alikana aliwapa Mabw Adan Omar Enow (sh1.506m), wakili James Gitau Singh(sh1.506m), Richard Abura (sh918,391), Monicah Nkina Saire (sh918,391), Eunice Kerich(sh498,391) na Samuel Njuguna(sh498,391).

Komen alikana mashtaka ya kuwalipa wanariadha walioshiriki katika michezo hiyo ya Olimpik  pesa za ziada ya Sh22.5 milioni kama marupurupu.

Bw Komen akiwa na wakili wake. Picha/ Richard Munguti

Bw Nzabu alikana akiwa meneja wa fedha aliidhinisha malipo ya Sh22.5 milioni kwa wanamichezo walioshiriki katika michezo hiyo ya kimataifa.

Mawakili Sagana na Kanyi Gakuya waliomba washtakiwa waachiliwe kwa dhamana.

Bi Kamau hakupinga ombi hilo ila alisema masharti ya dhamana yawe kama yale ya washukiwa walioshtakiwa Jumanne wiki hii. Alisema waliachiliwa kwa dhamana ya Sh1milioni pesa tasilimu.

Akasema Bw Ogoti, “Washtakiwa watalipa dhamana ya pesa tasilimu Sh1 milioni na kuwasilisha hati zao za dhamana kortini na wasiondoke Kenya bila idhini ya mahakama.”

Walioshtakiwa kwa kuhusika na kashfa hiyo na kuachiliwa Jumanne ni aliyekuwa katibu mkuu wizara ta michezo Bw Richard Titus Ekai , aliyekuwa msimamizi wa timu hiyo Bw Stephen arap Soi na aliyekuwa katibu wa kamati ya kitaifa ya michezo Bw Francis Kinyili Paul almaarufu F.K. Paul.

Mabw Wario, Komen na Nzabu walizuiliwa katika seli za mahakama huku watu wa familia zao wakishughulika jinsi ya kuwalipia dhamana.

Kesi itatajwa Novemba 16.