Habari

Salasya amkashifu Ruto kutokana na ripoti kuwa anajenga kanisa Ikuluni

Na CHARLES WASONGA July 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Mumias Mashariki Peter Salasya  amemkashifu vikali Rais William Ruto kutokana na ripoti kwamba anajenga Kanisa katika Ikulu ya Nairobi kwa gharama ya Sh1.2 bilioni.

Kwenye barua aliyomwandikia Rais na nakala yake akaiweka katika akaunti yake ya mtandao wa twitter, mbunge huyo anasema hatua hiyo ni kinyume na kipengele cha nane cha sheria kinachosema hamna dini ya serikali.

“Kwa hivyo, kwa kutumia pesa za umma kujenga Kanisa ndani ya Ikulu—nembo ya kitaifa—hiyo ni sawa na kuwabagua Wakenya waumini wa madhehebu mengine kama Kislamu, Kihindu, madhehebu ya kitamaduni na wasio amani uwepo wa Mungu,” Bw Salasya akasema.

“Je, atajenga msikiti, hekalu la Kihindi na maeneo ya ibada za kitamaduni karibu na kanisa hilo kuwafaa Wakenya wengine wasio wa dini ya Kikristo,” akauliza.

Bw Salasya alisema ujenzi wa kanisa hilo katika Ikulu ya Nairobi unaendeleza ubaguzi wa kidini nchini “jambo ambalo linakiuka katiba inayochukulia dini zote kuwa sawa na inapinga ubaguzi kwa misingi ya kidini.”

Habari kuhusu ujenzi wa kanisa hilo, ambalo litakuwa na uwezo wa kuwasitiri watu 8,000 kwa wakati mmoja, zilifuchuliwa mnamo Julai 4, 2025 kwenye magezeti ya “Taifa Leo” na “Daily Nation”.

Bw Salasya, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027, pia ametaja mradi huo kama ubadhirifu wa pesa za umma wakati hu ambapo Wakenya wanakumbwa na kero la kupanda kwa gharama ya maisha na kupungua kwa mapato.

“Wazazi hawawezi kumudu karo ya shule. Vijana hawana ajira. Hospitali hazina dawa na  Rais anatumia Sh1.2 bilioni, pesa za umma kujenga kanisa Ikulu. Huu ni usaliti mkubwa kwa mahasla ambao walimsaidia kupata ushindi akiahidi kuimarisha maisha yao,” akaeleza Bw Salasya.

Habari hizo pia zimeibua kero kubwa kwenye mitandao ya kijamii, haswa miongoni mwa Wakenya wa kizazi cha sasa, Gen Zs.

Lakini akiongea Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi alipokutana na viongozi kutoka kaunti ya Embu, Rais Ruto alikana madai kuwa Kanisa hilo linajengwa kwa pesa za umma.

“Hamna pesa zozote za umma zinazotumika katika ujenzi wa nyumba ya ibada katika Ikulu. Hizo ni porojo tu zisizo na ukweli wowote,” akaeleza.