Habari

Seneti kuamua jinsi Sonko atakavyojitetea

December 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

COLLINS OMULLO na IBRAHIM ORUKO

GAVANA wa Nairobi, Bw Mike Sonko, atajua Jumatano mfumo ambao maseneta watatumia kumpa nafasi ya kujitetea dhidi ya malalamishi yaliyosababisha madiwani wa kaunti hiyo kumtimua wiki iliyopita.

“Tutachapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali taarifa ya kualika maseneta kuhudhuria kikao maalumu,” Spika wa Seneti, Bw Kenneth Lusaka aliambia Taifa Leo jana Jumapili.

Bw Sonko alitimuliwa Alhamisi iliyopita kwa madai ya kukiuka Katiba, matumizi mabaya ya mamlaka na kuhusika katika visa vya uhalifu.

Jumatano, Bw Lusaka atawafahamisha maseneta kuhusu uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Nairobi na kupendekeza mfumo utakaotumika kusikiliza madiwani na Bw Sonko.

Sheria imetoa njia mbili: kusikilizwa na maseneta wote au kamati ya maseneta 11 ambao watasikiliza pande zote mbili na kisha kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwenye seneti na kupigiwa kura.

Mbinu ya kwanza ndiyo iliyotumiwa wakati uamuzi ulipotolewa kumtimua aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, almaarufu Baba Yao.

Mbinu ya kamati ilitumiwa kusikiliza malalamishi ya madiwani wa Kirinyaga dhidi ya Gavana Anne Waiguru, ambapo kamati hiyo ya seneti iliamua hapakuwa na sababu za kutosha kumng’oa mamlakani.

Japo Gavana Sonko ameahidi kupigana hadi mwisho, imebainika kuwa baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu katika chama cha Jubilee wamekuwa wakihimiza maseneta wamwondoe afisini.

“Nakuhakikishia kuwa uamuzi kuhusu hatima ya Sonko umefanywa. Wakuu ndani ya chama cha Jubilee wameamua kuwa ni lazima atimuliwe,” akasema seneta wa cheo cha juu katika seneti ambaye aliomba jina lake libanwe akihofia kusutwa kwa kufichua siri za chama.

Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata ambaye amepewa jina la ‘Rungu’ la Rais Uhuru Kenyatta ndani ya Seneti, alisema kuwa mchakato wa kumwondoa Bw Sonko utaendeshwa kwa kuzingatia sheria na ukweli wa madai ambayo yamewasilishwa dhidi yake.

“Seneti itaongozwa na sheria na mafunzo yaliyotokana na michakato ya kuwatimua magavana wengine ambao wamewahi kuletwa mbele ya Seneti,” akasema Bw Kang’ata ambaye alihusika pakubwa katika kumwokoa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru.

Akaongezea: “Jukumu la Seneti ni kuhakikisha kuwa wakazi wa Nairobi wanapata haki. Kesi hii itatathminiwa kwa makini bila kupendelea upande wowote.”

Tayari maseneta wanaonekana kugawanyika katika mirengo miwili. Mrengo wa kwanza ni ule wa maseneta wanaounga mkono ushirikiano wa Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambao umeapa kumtimua Bw Sonko. Mrengo wa pili unajumuisha maseneta wanaounga mkono Naibu wa Rais William Ruto ambao wanashikilia kuwa watasimama na Bw Sonko.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen amedai kuwa masaibu wa Bw Sonko yamefadhiliwa na Ikulu.