Habari

Seneti yaamuru Murang'a inyimwe fedha kutokana na 'ukaidi' wa gavana wake

September 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HUENDA kaunti ya Murang’a ikakosa kusambaziwa fedha kutoka Hazina ya Kitaifa mwaka huu ikiwa Waziri wa Fedha Ukur Yatani atatekeleza amri iliyotolewa na Kamati ya Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC).

Kamati hiyo imesema Alhamisi itamwagiza Bw Yatani kuzima pesa zozote kwa kaunti hadi Gavana Mwangi Wa Iria atakapokubali kufika mbele yake kujibu maswali kuhusu dosari katika matumizi ya jumla ya Sh24.5 bilioni ambazo Murang’a ilipokea kutoka Hazina ya Kitaifa kati ya Julai 2015 hadi Julai 2018.

Hii ni baada ya Bw Wa Iria kukaidi agizo la kufika mbele ya kamati hiyo ili atoe maelezo kuhusu makossa hayo yaliyoibuliwa katika ripoti za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali za miaka ya kifedha ya 2015/2016, 2016/2017 na 2017/2018.

Hii ni mara ya tatu kwa Bw Wa Iria kukaidi amri ya kutakiwa kufika mbele ya kamati ya CPAIC.

Majuma mawili yaliyopita mwenyekiti wa kamati hiyo Sam Ongeri aliamuru kwamba Gavana Wa Iria alikamatwe na kuwasilishwa mbele ya kamati yake na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai.

“Kwa kukataa kufika mbele ya kamati hii ni wazi kuwa Gavana Wa Iria hataki kuwajibikia matumizi ya fedha za umma. Kwa hivyo, kamati hii inamwandikia Waziri wa Fedha asisambaze fedha zingine kwa Kaunti ya Murang’a hadi gavana huyo atakapotii amri ya kamati hii,” akasema Prof Ongeri.

Seneta huyo wa Kisii alisema kamati yake imetoa agizo hilo kulingana na Kipengele cha 225 (4) cha Katiba na kipengele cha 96 cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM Act), zinazompa Waziri wa Fedha mamlaka ya kutosambaza fedha kwa serikali ya kaunti itakosa kuwajibikia matumizi ya fedha za umma.

“Hatuwezi kufumba macho yetu kwa hali kama hii ambayo ni kinyume cha Katiba. Kaunti ya Murang’a imepokea zaidi ya Sh24 bilioni kwa miaka mitatu ya kifedha. Sharti gavana Mwangi wa Iria awajibikie makosa katika matumizi ya fedha hizo yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali,” Profesa Ongeri akasisitiza.

Juzi Mahakama ilitoa agizo la kuzuia Seneti kumlazimisha Gavana Wa Iria kufika mbele ya kamati ya CPAIC baada ya gavana huyo kudai kamati hiyo ïlikataa ombi lake la kutaka apewa muda zaidi ajitarishe kufika mbele yake.

Mnamo Agosti 28, 2020, kamati ya CPAIC iliamuru Bw Mutyambai amsake na amwasilishe kwa nguvu mbele ya kamati hii mnamo Septemba 10, 2020 saa tatu na nusu za asubuhi ili atoe ufafanuzi kuhusu hitilafu katika matumizi ya fedha za umma.

Lakini kwenye barua aliyotuma kwa kamati hiyo, Bw Wa Iria alisema hangeweza kufika mbele ya kamati ya CPAIC kwa sababu Idara ya Afya imeamuru shughuli zote zisitishwe katika afisi za serikali ya kaunti ya Murang’a baada ya wafanyakazi wawili kupatikana na virusi vya corona.

Hata hivyo, Profesa Ongeri na maseneta Ochilo Ayacko (Migori) na Samson Cherargei (Nandi) walipuzilia mbali sababu hiyo wakisema kamati hiyo ilimwalika Bw Wa Iria tangu Junei 11, 2020.

“Alifaa kujiandaa mapema kufika mbele ya kamati hii, siku mojawapo wiki jana (wiki mbili zilizopita) baada ya ripoti ya maambukizi ya virusi vya corona kuchipuka katika afisi za kaunti hiyo,” alisema Bw Ayacko.