Habari

SENSA: Pwani walegea chumbani

November 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

ENEO la Pwani limo kwenye hatari ya kuendelea kubaki nyuma kimaendeleo na kisiasa kutokana na wakazi wake kukosa kutia bidii ya kuzaa watoto wengi.

Hii ni baada ya takwimu za hesabu ya watu zilizotolewa jana kuonyesha kuwa kaunti tatu za Pwani ni kati ya tano ambazo zinavuta mkia kwa kuwa na idadi ndogo zaidi ya watu.

Hii inamaanisha kuwa Pwani itaendelea kupata mgao wa chini wa fedha za maendeleo, na pia usemi wake utazidi kuwa hafifu katika masuala ya kisiasa.

Lamu inashika mkia kote nchini, Tana River imo katika nafasi ya 44 huku Taita Taveta ikitosheka kuwa nambari 43.

Kaunti za Isiolo na Samburu kutoka Mashariki zinafuatana katika nafasi za 46 na 45.

Kulingana na takwimu za matokeo hayo, Kaunti ya Lamu ina watu 143,920 pekee, Tana River 315,943 na Taita Taveta 340,671.

Baadhi ya wakazi wa Pwani waliohojiwa na Taifa Leo walitilia shaka matokeo hayo wakisema kuna wengi ambao hawakuhesabiwa.

Mkazi mmoja wa Taita Taveta naye alisema wazaliwa wengi wa kaunti hiyo hasa wanawake wameolewa nje ya kaunti hiyo ndiposa idadi ya wakazi iko chini.

Hata hivyo kaunti za Kilifi na Mombasa zilijizatiti ikilinganishwa na kaunti nyingine za Pwani baada ya matokeo hayo kuonyesha kuwa kuna watu milioni 1.4 Kilifi na milioni 1.2 Mombasa.

Kuwepo kwa idadi ndogo ya watu katika kanda ya Pwani kumepelekea viongozi kueleza hofu ya eneo hilo kukosa kuendelea maendeleo.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na maendeleo katika kanda ya Pwani, Hassan Mwakimako alisema kuwa matokeo hayo yatarudisha nyuma eneo hilo iwapo serikali itakumbatia mfumo wa kugawa fedha kulingana na idadi ya watu.

“Kunaweza kuwa na sababu tofauti za kuwepo kwa matokeo hayo ya chini katika kaunti za Pwani lakini suala kuu ni kuwa kanda ya Pwani itaendelea kutengwa kimaendeleo kama ambavyo ilivyokuwa siku za nyuma,” akasema Prof Mwakimako.

Kwa upande wake, Katibu mtendaji wa Baraza la Maimamu na Wahubiri (CIPK), Sheikh Mohammed Khalifa alisema kuwa kuna uwezekano kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawakuhesabiwa.

Kwa upande mwingine, kaunti za Nairobi, Kiambu, Nakuru, Kakamega na Bungoma ndizo zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu.

Kulingana na matokeo hayo yaliyotolewa jana, Kaunti ya Nairobi ambayo ndio jiji kuu la nchi ina watu milioni 4.3 ikifuatwa na Kiambu yenye watu 2.4 milioni.

Kaunti ya Nakuru yenye watu 2.1 milioni inashikilia nafasi ya tatu, huku kaunti mbili kutoka eneo la Magharibi – Kakamega (1.8 milioni) na Bungoma (1.6 milioni) zikishikilia nafasi za nne na tano mtawalia.