Habari

Serikali inaweza kuzima mitandao kulinda usalama wa nchi – Kabogo

Na TITUS OMINDE  January 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali William Kabogo, ametahadharisha kuwa serikali inaweza kuzima mitandao ya kijamii endapo kutakuwa na tishio kwa usalama wa kitaifa.

Akizungumza jijini Eldoret wakati wa Kongamano la Kimataifa la Kulinda Data katika Eldoret Sports Club, Bw Kabogo, alisema kwamba serikali ina uwezo wa kuzima mitandao ya kijamii ili kuwazuia Gen Z kuitumia vibaya.

Bw Kabogo ameeleza kusikitishwa kwa serikali na mienendo ya vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kusambaza picha za watu maarufu hasa viongozi wa kisiasa wakiwa kwenye majeneza mitandaoni.

Waziri Kabogo alisema kuwa serikali inaweza kuzima mitandao ya kijamii kukiwa na tishio kwa usalama wa kitaifa.

Akizungumza jijini Eldoret wakati wa Kongamano la Kimataifa la Kulinda Data Eldoret Sports Club, Bw Kabogo alitaja kisa cha Rwanda wakati vyombo vya habari vilitumiwa kuchochea mauaji ya kimbari.

Bw Kabogo alibaini kwamba serikali ina uwezo wa kuzima mitandao ya kijamii ili kuwazuia Gen Z kuiumia vibaya.

“Uwezo upo endapo tutahisi kuwa kuna tishio kwa usalama wa taifa. Kwa mfano, tunajua kilichotokea Rwanda wakati redio zilitumiwa kuchochea mauaji ya kimbari. Hilo likitokea tutazima mitandao ya kijamii,” alisema Bw Kabogo.

Bw Kabogo alisema tabia ya vijana kutumia vibaya mitandao ya kijamii inawasumbua viongozi wanaolengwa huku akiwasihi vijana kuachana na tabia hiyo ambayo aliitaja kama dharau kwa viongozi.