Serikali kutafutia mitishamba ya Pwani masoko katika nchi za ng’ambo
SERIKALI itasaidia wenyeji wa Kaunti ya Tana River kutafuta soko la kimataifa kwa dawa zao za kienyeji na bidhaa za urembeshaji.
Katibu wa Wizara anayesimamia Turathi za Kitaifa, Bi Ummi Bashir, amesema idara hiyo kwa ushirikiano na Serikali ya Tana River pia imeanza mikakati ya uchoraji wa ramani ya maeneo ya turathi za kitaifa katika kaunti hiyo.
“Kuna aina ya udongo hapa ambao ninaambiwa unaweza kupunguza kasi ya mtu kuzeeka. Watu ulimwenguni wako hulipia gharama kubwa kupata vitu kama hivyo, ilhali hapa Tana River inachukuliwa kama ni udongo wa kawaida. Tutaitafutia soko,” akasema Bi Bashir mjini Ngao, Tana River, wakati wa uzinduzi wa makavazi ya kwanza ya kaunti hiyo.
Katibu alisema makavazi hayo ni kati ya mikakati ambayo serikali imeweka ili kutanua sekta ya utalii eneo la Pwani.
Bi Bashir pia alidokeza kuwa serikali itapiga jeki serikali ya kaunti katika pilkapilka za kusaka rasilimali za kukarabati vituo vya turathi, kwa lengo la kuviimarisha na kuvitambua rasmi kama vivutio vya watalii na wanaikiolojia kote duniani.
Kauli yake iliungwa mkono na Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, ambaye alikariri kuwa kaunti hiyo ni kitovu cha historia pevu ambayo inahuisha matukio yaliyorekodiwa katika vitabu vya kumbukumbu.
Gavana Godhana alisema kaunti hiyo ina uwezo wa kuwa mojawapo ya vitovu vya utalii barani Afrika ikiwa serikali na washikadau watawekeza ipasavyo katika juhudi za kuboresha maeneo hayo ya kihistoria.
“Ilikuwa katika gereza la Hola ambapo wafungwa wa vita vya uhuru waligoma kula na wakapigwa virungu hadi kufa. Kisa hicho kilichochea gumzo kubwa kwenye kongamano la kwanza la Lancaster House (jijini London, Uingereza), ambalo ndilo lilikuwa maskani ya mijadala iliyoishia kwa mkoloni kuondoa udhibiti wake na taifa letu kujinyakulia uhuru. Lakini sehemu hiyo ya historia huwa haizungumziwi, inahitaji kuwekwa wazi,” alieleza Bw Godhana.
Wakazi wameshabikia makavazi hayo ya kwanza kabisa Tana River kama urithi wao, na kuhimiza watalii wa humu nchini na kigeni kuyatembelea na kujifunza kuhusu historia yao.
Kituo hicho kikongwe cha miaka 120 kilichozinduliwa mjini Ngao kimehifadhi pia hadithi za jinsi wenyeji walipambana na mkoloni kupinga juhudi za kuanzisha Ukristo katika eneo hilo.
Vile vile, kuna sanaa ambazo zimetundikwa kama maonyesho kwenye jumba la makumbusho. Sanaa hivi ni pamoja na mtumbwi wa zaidi ya miaka 100, mitego ya zamani ya uvuvi, sufuria na sahani zilizotumiw na watu wa kale.