Serikali ya Kaunti ya Nairobi yapendekeza sheria ya kuthibiti idadi ya matatu, nauli
SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imependekeza sheria zinazolenga kuboresha sekta ya uchukuzi kwa kuthibiti idadi ya matatu katika kila barabara na nauli.
Chini ya sheria hizo mpya, wizara ya kaunti inayosimamia sekta ya uchukuzi itahakikisha kuwa idadi ya gari katika kila barabara inaongozwa na mahitaji, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari.
Kando na hayo, sheria hiyo pia inalenga kudhibiti kelele Katikati mwa jiji kwa kuhakikisha kuwa madereva hawaweki muziki wakiwa eneo la CBD.
Mpango huu pia unalenga kupambana na kero ya kelele unaoathiri biashara, taasisi za elimu na wakazi katikati mwa jiji.
Kwa upande mwingine, makondakta hawataruhusiwa kupiga kelele kuwaita wateja. Badala yake, watahitajika kutumia mabango maalum yanayoonyesha maelezo ya wanakoenda na nauli.
Magari ya uchukuzi pia yatahitajika kuondoka katika vituo vyao kufika saa nne usiku ili kutoa nafasi ya kusafisha jiji kila usiku.