Serikali yageukia KDF kukamilisha miradi iliyokwama
JESHI la Kenya (KDF) limejiunga na sekta ya ujenzi kuhakikisha miradi mikubwa ya serikali inakamilika serikali ikipanga kukamilisha miradi ya mabilioni iliyokwama.
Kampuni mpya ya Ulinzi Construction Company imepatiwa zabuni za kujenga barabara, hospitali na viwanja vya michezo, huku jeshi likisimamia miradi mingi ya serikali kuhakikisha ufanisi na kukamilika kwa wakati.
Kulingana na Katibu wa Wizara ya Ulinzi, Dkt Patrick Mariru, jeshi linafuatilia miradi zaidi ya 72 mikubwa ya serikali ambayo inatarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2027.
“Tunachopatia kipaumbele ni ufanisi na kukamilika kwa miradi ili wananchi wapate thamani ya fedha zao,” alisema Dkt Mariru Novemba 17, 2025 wakati wa kuzinduliwa kwa ujenzi wa hospitali ya pili ya rufaa ya Moi (MTRH) inayogharimu Sh50 bilioni huko Eldoret.
Ujenzi wa hospitali hiyo yenye vitanda 4,000 katika eneo la Kiplombe, nje kidogo ya mji wa Eldoret, unafuatia idhini kutoka serikali na washirika wa maendeleo kusaidia kupunguza msongamano katika hospitali ya sasa yenye vitanda 1,405.
Awamu ya kwanza ya hospitali hiyo ya rufaa itakuwa na vitanda 2,000 na inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.Wizara ya Afya na usimamizi wa MTRH walikiri kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi kutokana na changamoto za awali, ikiwemo ukosefu wa fedha na kuingiliwa kisiasa kwa miradi ya kitaifa.
“Ujenzi wa hospitali hiyo utakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kukuza utalii wa matibabu na kuvutia wateja wa kikanda na kimataifa,” alisema Waziri wa Afya Aden Duale, huku akilaani kuingiliwa kisiasa kwa miradi muhimu ya maendeleo.
Kampuni ya China, China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Company Limited, ndiyo inayojenga hospitali hiyo, huku KDF ikisimamia mradi kuhakikisha unakamilika kwa wakati.“Jeshi la KDF litakuwepo kuhakikisha hakuna uzembe,” alisema Bw Duale, huku akibainisha kwamba KDF inasimamia miradi kama hii kote nchini.
Bw Duale pia alisisitiza ahadi ya Wizara ya Afya kutoa huduma za msingi na za rufaa ili kupunguza msongamano katika hospitali za rufaa.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba kukamilika kwa miradi muhimu kama hii kumechukua muda mrefu kutokana na siasa hasi. Ni wakati muafaka wa kutenganisha siasa na maendeleo yenye maana,” alisema, huku akiwataka Wakenya zaidi kujisajili na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Alibainisha kuwa Wakenya milioni 27.5 tayari wamesajiliwa huku Kaunti ya Mombasa ikiongoza, ikifuatiwa na Bomet, Elgeyo Marakwet, Nandi na Uasin Gishu.