Habari

Serikali yapiga marufuku aina 17 za unga wa mahindi

January 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DIANA MUTHEU

SERIKALI imepiga marufuku aina 17 za unga wa mahindi ikisema ni hatari kwa afya ya binadamu.

Shirika la Ubora wa Bidhaa (KEBS) lilieleza kuwa uchunguzi wake ulionyesha unga huo una viwango vya juu vya sumu hatari ya kuvu (aflatoxin), na likaagiza kampuni husika ziuondoe kwenye maduka yote.

KEBS ilitaka aina hizo za unga zikome kuuzwa madukani kote na ikawatumia wafanyibiashara wa maduka makubwa barua pepe ikiwataka watume aina ya unga walio nao na idadi yake ili kuwezesha shirika hilo kuukusanya na kuuondoa madukani.

KEBS ilitangaza kuwa mfanyibiashara yeyote ambaye ataendelea kuuza aina hizo za unga zilizopigwa marufuku atakamatwa.

“Kuuza bidhaa zilizopigwa marufuku ni kinyume cha sheria na watakaokiuka masharti haya watachukuliwa hatua kali,” ripoti ya KEBS ikasema.

Aina hizo za unga ni African King kutoka kampuni ya African Lings Maize Millers, Unique wa Dosha Limited, Mlo kutoka Bidii Ltd, City Corn wa Central Afya Bora Millers, Sarafina unaotengenezwa na Century Millers, na Tosha wa Godmesa Foods and Allied Limited.

Zingine ni Shiba kutoka Grange Suba Millers, Hakika Best kutoka Halisi Maize Mills, Budget unaotengenezwa na Karibu Flour Mills Ltd, Wema kutoka kampuni ya Luma Millers Limited, Jomba wa Machakos Millers, Adardere Mupa kutoka Mbaitu Maize Milling na Afya kutoka Meru Multi-purpose Co-operative Society Ltd.

Pia kuna Uzima wa kampuni ya Sigose Farm Company Limited, Sungura kutoka Sungura Unga Miller Ltd, Dola kutoka Eldoret Grain Millers na Tetema kutoka kampuni ya Eldoret Grains Limited.

Mnamo Novemba 2019 KEBS ilipiga marufuku uuzaji wa unga wa Kifaru kutoka kampuni ya Alpha Grain Limited kutokana na viwango vya juu vya kuvu.

Katika msako huo wa mwaka 2019 unga wa Dola pia ulipigwa marufuku pamoja na ule wa Starehe unaotengenezwa na kampuni ya Pan African Grain, Nairobi 210 (Two Ten) kutoka Kenblest Limited Thika na Jembe kutoka Kensalrise Limited Eldoret.

Shirika hilo liliagiza kampuni hizo zikome kutengeneza bidhaa hizo na zile zilizo sokoni zitolewe madukani.