Habari

Serikali yapiga marufuku masomo ya ziada wakati wa likizo ya Disemba

Na WINNIE ATIENO November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI imepiga marufuku masomo ya ziada wakati wa likizo ya Disemba, siku chache baada ya shule kutuma barua kwa wazazi zikiwataka wanafunzi kurejea darasani wiki ijayo baada ya kukamilika kwa mitihani ya KPSEA na KJSEA.

Mtihani wa KPSEA ulimalizika wiki iliyopita huku ule wa KJSEA ukikamilika Novemba 3, 2025.

Waziri wa Elimu Bw Julius Ogamba alisema shule haziruhusiwi kufanya masomo ya ziada wakati wa likizo.

“Ni kinyume cha sheria kufanya masomo ya ziada baada ya shule kufungwa. Tutatoa onyo rasmi kuhusu hilo kwenye barua zitakazosambazwa shuleni. Maafisa wetu wa elimu walioko mashinani watafanya ukaguzi ili kuhakikisha hakuna shule inayoendelea na masomo wakati wa likizo,” alisema Bw Ogamba kwenye mahojiano na Taifa leo Dijitali.

Wiki iliyopita, Muungano wa Wazazi Nchini (NPA) ilitoa tahadhari kufuatia taarifa kwamba shule kadhaa nchini zimetuma barua kwa wazazi kuwajulisha kuhusu masomo ya ziada.

Kulingana na muungano huo, baadhi ya shule za msingi na sekondari zimetuma barua kwa wazazi kuwatayarisha watoto wao kwa masomo ya ziada wakati wa likizo ya Disemba.

Aidha mwenyekiti wa muungano huo Bw Silas Obuhatsa alisema wazazi pia waagizwa kulipa ada ya masomo hayo ambayo yataanza rasmi wiki ijayo baada ya kumalizika kwa mitihani ya kitaifa ikiwemo KPSEA, KJSEA na ile ya kidato cha nne (KCSE).

Bw Obuhatsa alisema wazazi kutoka sehemu mbali mbali nchini wamejulisha afisi yake kuhusu uhalifu huo akiitaka wizara kuwachukulia hatua kali za kisheria shule hizo.

“Shule kadhaa zimewaagiza wazazi kuanza kulipa ada ya masomo ya ziada kuanzia Jumanne wiki ijayo, wakilenga wanafunzi wa Gredi ya 1 hadi 9 yakipangwa. Shule nyingi zimeamua kutofunga kulingana na kalenda ya elimu. Badala yake, zimepanga kuendelea na masomo mara tu baada ya mitihani kumalizika,” alisema Bw Obuhatsa.

Aliwashtumu walimu wakuu ambao wamepanga masomo hayo akisema wanatamaa ilhali wanalipwa mishahara.

Wiki mbili zilizopita, Wabunge walimtaka Waziri Ogamba kutoa maagizo makali kwa shule kuhakikisha zinafuata maagizo ya wizara.

Hii ni kufuatia malalamiko kutoka kwa wazazi na wadau wa elimu kwamba baadhi ya wanafunzi, wakiwemo watoto wadogo wa miaka saba, wanalazimishwa kwenda shuleni alfajiri ya saa kumi.

“Shule zikikaidi maagizo ya wizara, hatua kali za kisheria zichukuliwe,” alisema Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kisii, Bi Dorice Donya.

Aliitaka wizara kushirikiana na Wizara ya Usalama wa Ndani kuhakikisha maagizo yanatekelezwa na shule zitakazokaidi zinachukuliwa hatua kali.