Serikali yapunguza bei ya petroli, dizeli na mafuta taa… kwa senti chache
SERIKALI imepunguza bei ya mafuta kwa senti chache hatua ambayo haitatoa afueni kwa Wakenya katika kipindi cha mwezi mmoja ujao, kuanzia Septemba 15 hadi Oktoba 14, 2025.
Kulingana na tangazo lililotolewa Jumapili na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Petroli (EPRA) bei ya petroli imepunguzwa kwa senti 79 kwa lita, dizeli imeshuka kwa senti 11 huku bei ya mafuta taa ikipunguzwa kwa senti 80 kwa lita ndani ya kipindi hicho.
Hii ina maana kuwa kuanzia Septemba 15 petroli, dizeli na mafuta taa zitauzwa kwa Sh184.53, Sh171.47 na Sh154.78, jijini Nairobi na viunga vyake.
Katika kipindi cha kati ya Agosti 15 na Septemba 14, 2025, petroli iliuzwa kwa bei ya Sh185.31, dizeli (Sh171.58) huku mafuta ikiuzwa kwa Sh155.58 jijini Nairobi na viunga vyake.
Epra ilisema bei hizo mpya zinajumuisha ushuru wa VAT wa kina cha asilimia 16 kulingana na hitaji la Sheria ya Fedha ya 2023, Sheria za Ushuru (zilizofanyiwa mageuzi) ya 2024 na ada nyinginezo zinazobadilishwa kila mara kulingana na mfumko wa bei.
Mamlaka hiyo ilieleza kuwa kupungua kwa bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kumechangiwa na kupungua kwa bei ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje kati ya Julai na Agosti mwaka huu.