Serikali yatangaza Shona kuwa kabila la 44 nchini
Na CHARLES WASONGA
WATU wa asili ya Shona ambao wamekuwa wakiishi nchini kwa miongo kadhaa bila kutambuliwa sasa wamepata afueni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuamuru watambuliwa kama raia wa Kenya.
Rais Kenyatta aliyapa makundi hayo mawili vyeti vya uraia Jumamosi wakati wa sherehe za Sikukuu ya Jamhuri Dei katika uwanja wa Nyayo, Nairobi.
Hatua hiyo imetoa nafasi kwa makundi hayo ya wachache kupata stakabadhi za utambulisho kama vile Kitambulisho cha Kitaifa na vyeti vya kuzaliwa.
Waziri wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i alitangaza kuwa sasa jumla ya watu 3,500 wa jamii ya Shona wanaoishi katika Kaunti ya Kiambu watakuwa huru kuanza harakati za kusaka stakabadhi zote za kuwatambulisha kama Wakenya.
“Ama kwa hakika ningependa kutangaza kuwa kuanzia leo (jana Jumamosi) Shona ni kabila la 44 nchini Kenya,” akasema Dkt Matiang’i.
Watu wa jamii hiyo ambao walikuwa wakifuatilia tangazo hilo katika Kanisa la Gospel of God, Nairobi walifurahia hatua hiyo wakisema sasa itawaondolea ubaguzi ambao wamekuwa wakiupitia kwa miongo kadha.
Mwinjilisti Pater Mwawa alisema hatua hiyo ni kama kuzaliwa upya kwa jamii hiyo na kupitia kutimia kwa juhudi zao za miaka mingi za kutaka kutambuliwa.
“Japo tumeishi kwa amani nchini Kenya kwa miaka mingi, tumepitia changamoto si haba. Tumekosa huduma za serikali kwa kukosa stakabadhi za uraia kwani hatukutambuliwa kama Wakenya licha ya kwamba wengi wetu tumezaliwa humu Kenya. Sasa tumefurahi kwamba tutashirikiana kikamilifu na Wakenya wengine katika ujenzi wa taifa,” akasema.
Washona waliasili nchini Kenya kama Wamishenari kutoka Zimbabwe. Lakini hawakurejea kwao na badala yake wakaamua kuishi nchini. Wengi wao wanaishi katika maeneo ya Kinoo na Kiambaa katika Kaunti ya Kiambu ambako wanajishughulisha na kazi za mikono kama utengenezaji vikapu.
Naibu Mkurugenzi wa Tume ya Haki za Kibinadamu Nchini (KHRC) Davis Malombe alipongeza hatua ya kutambuliwa kwa Washona akisema imetokana na kampeni ya miaka minne ambayo imekuwa ikiendeshwa na tume hiyo kutaka jamii hiyo itambuliwe.