Habari

Serikali yatangaza ufunguzi wa shule tano za Boni

November 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

NI afueni kwa mamia ya wanafunzi wa shule za msingi zilizoko Boni, Kaunti ya Lamu baada ya serikali ya kitaifa kutangaza kufunguliwa kwa shule hizo ifikapo Januari mwakani.

Shule hizo tano za Basuba, Milimani, Mangai, Mararani na Kiangwe zililazimika kufungwa kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita kufuatia uvamizi wa mara kwa mara uliokuwa ukitekelezwa na magaidi wa al-Shabaab ambao waligeuza msitu wa Boni kuwa ngome ya uvamizi.

Akizungumza akiwa eneo la Kiangwe wakati wa ziara yake kwenye msitu wa Boni, Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata, amesema operesheni ambayo imekuwa ikiendelea ya kuwasaka na kuwamaliza wafuasi wa kundi la al-Shabaab ndani ya msitu huo imezaa matunda kwani amani na utulivu umekuwa ukishuhudiwa eneo hilo kila kuchao.

Bw Elungata amesema serikali imeafikia kuzifungua shule zote za msitu wa Boni kufikia Januari 1, 2020, ili watoto wa jamii ya walio wachache wapate elimu wakiwa vijijini mwao.

Mshirikishi wa Usalama Ukanda wa Pwani, John Elungata (wa pili kushoto) akiwasili eneo la Kiangwe, msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu. Anasema serikali itafungua shule zote tano za msitu wa Boni kufikia Januari 2020. Picha/ Kalume Kazungu

Tangu shule za eneo hilo zilipofungwa, wanafunzi wa jamii ya Waboni wamekuwa wakihangaika kwa kusafirishwa mbali na karibu hadi mjini Kiunga na pia Mokowe ili kupata elimu.

Bw Elungata ameitaka Tume ya Kuajiri Walimu nchini (TSC) kupeleka walimu wa kutosha kwenye vijiji vya msitu wa Boni ili kuhudumia shule hizo pindi zikishafunguliwa.

Amewahakikishia walimu watakaopelekwa eneo la msitu wa Boni usalama wa kutosha, akisisitiza kuwa walimu hao wataishi ndani ya kambi za walinda usalama na kwenda shuleni kufunza kila siku.

“Usalama umeimarishwa msituni Boni na Kaunti ya Lamu kwa jumla. Tumefika hapa leo kuwatangazia rasmi kwamba shule zote tano zilizofungwa kwenye msitu wa Boni tutazifungua kufikia Januari mwaka ujao. Tayari tumejadiliana na maafisa wa TSC ili kuona kwamba walimu wa kutosha wanaletwa hapa kusomesha watoto wetu. Usalama wa walimu hao uko juu yetu. Wasiwe na shaka. Watakuwa wakilala na kula ndani ya kambi za jeshi na polisi zilizoko hapa. Lao litakuwa tu kwenda shuleni kufunza mchana na kisha kurudi kambini jioni. Tushirikiane kufaulisha mpango huo,” akasema Bw Elungata.

Amani na utulivu

Gavana wa Lamu, Fahim Twaha kwa upande wake ameishukuru serikali ya kitaifa kwa juhudi zake katika kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa Lamu.

Bw Twaha amewataka wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni mara taasisi hizo zitakapofunguliwa tena Januari.

Amesema serikali yake pia itashirikiana kwa karibu na serikali ya kitaifa ili kufaulisha masomo kwenye msitu wa Boni.

“Nina furaha tele kwamba serikali imeafikia kuzifungua shule za msitu wa Boni. Nafurahia juhudi za serikali katika kupigana na wahalifu kwenye msitu wa Bonin a kuleta amani kote Lamu. Ushauri wangu kwa wazazi ni kwamba wahakikishe watoto wao wanafika shuleni kusoma punde shule hizo zitakapofunguliwa ifikapo Januari,” akasema Bw Twaha.

Nao wabunge, Athman Sharif (Lamu Mashariki), Stanley Muthama (Lamu Magharibi) na Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Lamu, Bi Ruweida Obbo wamesifu uamuzi wa serikali ya kitaifa wa kuzifungua shule za msitu wa Boni na kuutaja mpango huo kujiri kwa wakati ufaao.

“Elimu pekee ndiyo itakayonasua jamii yetu kutoka kwa umaskini. Ni ombi langu kwamba huku serikali ikifanya jitihada hizo, jamii yenyewe itaamka kwa kuzingatia zaidi masomo ya watoto wao kwa manufaa yao ya siku za usoni,” akasema Bw Sharif.