Shida kivukoni kufuatia feri 2 kuondolewa
Na MOHAMED AHMED
MAELFU ya watumizi wa feri katika kivuko cha Likoni wanatarajiwa kupambana na msongamano mkubwa kufuatia kuondolewa kwa feri mbili.
Shirika la Huduma za Feri (KFS) limeziondoa feri ya Mv Nyayo na Mv Likoni kivukoni hapo.
Maafisa wa KFS waliozungumza na Taifa Leo walifichua kuwa feri hizo mbili ziliondolewa baada ya kuleta shida za kimitambo.
Wadokezi wetu walieleza kuwa propela ya feri ya Mv Likoni imeharibika hivyo basi kupelekea kuondolewa kwake.
“Mafundi wetu walijaribu kutengeneza feri hiyo lakini wakashindwa hivyo basi inatarajiwa kupelekwa African Marine and General Engineering Company (Amgeco) kwa ajili ya marekebisho,” akasema afisa mmoja wa KFS ambaye hakutaka kutajwa.
Feri hiyo ilikuwa imeondolewa kuanzia Jumatatu ikisubiri kutengenezwa. Afisa wa mawasiliano ya KFS Bw Aaron Mutiso alithibitisha kuwa feri hiyo imeondolewa kwa ajili ya marekebisho na kusema kuwa itarudishwa hivi karibuni.
Aidha, feri ya Mv Nyayo nayo iliondolewa jana baada ya KFS kueleza kuwa itapelekwa kwa marekebisho ya kawaida.
Wiki jana, KFS ilikuwa imetangaza kuwa feri hiyo itaondolewa lakini ikaendelea kuhudumu hadi jana ndipo ikaondolewa. Feri ya Mv Nyayo ni miongoni mwa zile zilizohudumu kwa zaidia ya miaka 30 katika kivuko cha Likoni zikisaidiana na nyingine kuhudumia zaidi ya watu 300, 000 na magari zaidi 6, 000 kila siku.
Kufuatia kuondolewa kwa feri hizo mbili, wenye magari walikaa saa nyingi jana asubuhi kabla ya kuvuka kutoka upande wa Likoni.
Hali hiyo ilisababishwa na kubakishwa kwa feri tatu pekee kivukoni hapo ikiwemo ile ya Mv Jambo, Mv Kwale na Mv Kilindini.
Kubakishwa kwa feri hizo tatu kulipelekea maafisa wa KFS kuwa na wakati mgumu kupambana na umati mkubwa wa watu na msongamano wa magari ambayo yalikuwa yanang’ang’ania kuingia.