HabariSiasa

Shinikizo Ruto ajiuzulu zashika kasi

March 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

HUKU mjadala kuhusu vita dhidi ya ufisadi ukizidi kupamba moto nazo kambi tofauti za kisiasa zikizidi kushambuliana kuhusu jinsi vita hivyo vinavyoendeshwa, baadhi ya wabunge tayari wanawazia kumng’oa Naibu Rais William Ruto afisini, kutokana na jinsi anavyovipinga.

Wabunge kutoka maeneo ya Mlima Kenya na Ukambani wameeleza kughadhabishwa kwao na Dkt Ruto, wakionyesha dalili za kuwasilisha mswada wa kutokuwa na imani naye.

Wakiwa katika eneobunge la Kathiani Jumamosi, zaidi ya viongozi 10 walimvamia Naibu Rais kuhusiana na jinsi ambavyo amekuwa akikosoa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusu jinsi inavyoendesha vita dhidi ya ufisadi, baadhi yao wakipendekeza kuwa itakuwa afadhali kumng’oa kutoka afisini.

“Kipengee cha 147 kwenye katiba kinasema wewe ni msaidizi wa Rais na ukicheza na kipengee cha 150 kinasema ukifanya mambo hivi hivi, tukinusa tu, (tunakutupa) nje, tunakung’oa mamlakani.

“Serikali ni ya Uhuru, si ya Uhuru na mtu mwingine, Urais haugawanywi, sisi hatuna Rais wawili. Wakati huu president si mwizi, mwizi yuko kitandani karibu naye,” akasema mbunge wa Kangema Muturi Kigano.

Mbunge mwenzake wa Kathiani Robert Mbui naye alimtaka Rais Kenyatta kumfuta kazi “mshirika wake wa karibu zaidi kisiasa” ambaye alimrejelea alipokuwa akionya watu fisadi wiki iliyopita, ama awape wabunge fursa ya kumng’oa.

“Ninataka kuuliza Rais, si unajua yule ‘mshirika wa kisiasa wa karibu zaidi’ wako ni nani? Rudisha huyu mtu nyumbani ama utuambie tumng’oe mapema ili ufanye kazi,” akasema Bw Mbui.

Wabunge hao walikuwa wakizungumza katika hafla ambapo wabunge wengine kama vile Maina Kamanda (Starehe), Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Paul Koinange (Kiambaa), Dan Mwachako (Wundayi) na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Dennis Waweru walikuwapo pia.

Viongozi hao walimkashifu Dkt Ruto kuhusu suala la sakata ya pesa zinazodaiwa kuporwa kwenye miradi ya mabwawa ya Kimwarer na Arror, kufuatia matamshi yake kuwa si Sh21 bilioni zinazokosekana ila ni Sh7 bilioni zinazotiliwa shaka.

Bw Waweru alisema, “Kwa hivyo, hawa wakora wa mabwawa ambao wanaogopa DCI wameiba pesa sawa na zile tunazolipia watoto masomo Kenya nzima na kwa hivyo leo tunataka kuwaambia wajiuzulu, kwa sababu wameiba pesa za watoto wetu.”

Matamshi ya mbunge huyo yaliungwa mkono na Bw Mwachako ambaye alisema “Yule atakayetajwa kuwa amekula pesa za mwananchi, wacha akae kando uchunguzi ufanyike.”

Bw Koinange, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu usalama naye alisema pesa zote za umma ambazo zimeporwa zitafikiwa na kurejeshwa.

Alhamisi, mbunge huyo alikuwa ametetea Idara ya DCI kuhusu jinsi ambavyo imekuwa ikivamiwa na baadhi ya wanasiasa, akisema ataongoza juhudi za kuitetea ili iongezwe pesa zaidi ili iimarishe kazi yake.

Seneta wa Siaya, Bw James Orengo alipendekeza Dkt Ruto aondoke serikalini kwa kutofautiana na misimamo ya Rais Kenyatta.

“Kama Ruto anamtambua Uhuru Kenyatta kama Rais wa Kenya kwa kweli, lazima pia ajitokeze kusema kuna wizi. Lakini kama Uhuru anaesema hivi na yeye anasema vingine, wanafanya kazi pamoja kweli? Tunataka Uhuru asiogope. Ukiwa na number two lazima ufanye ile kazi unayotaka naye awafanyie wananchi, ukiacha hiyo unakuwa msaliti.”