Shirika la Reli lasitisha safari ya usiku ya Mombasa kuja Nairobi
SHIRIKA la Reli limesema hakutakuwa na safari ya Mombasa kuja Nairobi Julai 6, 2025 saa nne usiku.
Kulingana na taarifa katika mitandao yao ya kijamii, shirika hilo linasema kuna hitilafu za kimitambo zilizolazimu hatua hiyo.
“Tunasikitika kujulisha umma kwamba kwa sababu ya hitilafu za kimitambo, hakutakuwa na safari ya kutoka Mombasa hadi Nairobi ya saa nne usiku Julai 6, 2025; tunaomba radhi kwa kusababisha usumbufu,” ikasema taarifa hiyo fupi.
Haya yanajiri huku kukiwa na ripoti kwamba kundi la vijana waliohudhuria tamasha Diani limezuiwa na maafisa wa usalama kusafiri kuja Nairobi, hatua ambayo imechukuliwa kuwa ya kujaribu kudhibiti maandamano ya Saba Saba.
Vijana hao ambao walihudhuria tamasha la Diani Summer Tide Festival wanadaiwa kusimamishwa katika barabara Dongo Kundu karibu na Likoni, Mombasa.
Ilidaiwa kwamba walikuwa wanaenda kuabiri treni ya saa nane mchana. Waliohojiwa walisema polisi waliwaambia kwamba wakiruhusiwa kupita wataenda kushiriki maandamano ya Saba Saba Nairobi.