Habari

Siasa za ubabe! Kalonzo sasa amgonga Ruto

Na NDUBI MOTURI December 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amepuuza mashambulizi kutoka kwa Rais William Ruto, akimlaumu kwa kupotosha kimakusudi rekodi yake katika utumishi wa umma.

Haya yanajiri huku ushindani wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 ukizidi kupamba moto.

Kwa wiki kadhaa sasa, Rais Ruto amekuwa akitumia mikutano ya hadhara na majukwaa ya kisiasa kuhoji mchango wa Bw Musyoka katika maendeleo, mara kwa mara akimtaka “aonyeshe rekodi yake ya maendeleo” ya kile anachosema ni zaidi ya miaka 40 serikalini.

Mashambulizi hayo yanalenga kumsawiri makamu rais huyo wa zamani kama mwanasiasa ambaye, kwa mujibu wa Rais Ruto, hakuwaletea Wakenya wa kawaida manufaa ya moja kwa moja licha ya kuhudumu serikalini kwa miaka mingi.

Hata hivyo, katika majibu makali, Wiper Patriotic Front ilikanusha madai hayo, ikisema kauli za rais ni juhudi za kupotosha historia ya maendeleo ya Kenya na siasa za mapema dhidi ya kinara huyo wa upinzani.

“Huu si mjadala wa haki kuhusu maendeleo. Haya ni mshambulizi wa kisiasa yanayotokana na kuhisi kushindwa,” alisema Katibu Mkuu wa Wiper, Seneta Shakila Abdalla, kupitia taarifa. “Rais Ruto anajifanya kuwa maendeleo ni mali binafsi ya mtu mmoja au utawala mmoja.”

Seneta Abdalla alisema rekodi ya Bw Musyoka haiwezi kupuuzwa kwa vijembe jukwaani, akisisitiza kuwa mchango wake serikalini unapaswa kuangaliwa kwa mtazamo wa uongozi wa pamoja na mipango ya muda mrefu. Alirejelea wadhifa wake wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki alipokuwa makamu wa rais, na awali akiwa waziri serikalini.

“Kalonzo Musyoka alikuwa mhimili muhimu wakati wa kubuniwa kwa Ruwaza ya 2030, ambapo taifa hili liliweka ramani kabambe zaidi ya maendeleo kuwahi kuwa nayo,” alisema. “Barabara, taasisi na mageuzi zilipangwa na kufadhiliwa wakati huo, hazikuibuka juzi kwa sababu ya kampeni.”

Chama hicho kilipinga vikali madai ya rais kwamba viongozi wa upinzani walihudumu serikalini kwa miongo mingi bila kuleta maendeleo, kikisema hoja hizo zinapuuza jinsi miradi mikubwa hupangwa, kufadhiliwa na kutekelezwa kwa miaka mingi na tawala tofauti.

“Maendeleo ni haki ya kikatiba ya wananchi, si hongo ya kampeni wala hisani ya rais aliye mamlakani,” alisema Seneta Abdalla. “Tunachoshuhudia sasa ni jaribio la kuandika upya historia ili mtu mmoja aonekane kama ndiye mpangaji wa pekee wa maendeleo.”

Wiper pia ilimlaumu rais kwa kujipatia sifa za miradi iliyoanzishwa kabla ya utawala wake, hasa katika eneo la Kusini Mashariki mwa nchi. Seneta Abdalla alitaja barabara ya Kibwezi–Mutomo–Kitui–Bondoni, akisema ilianzishwa na kufadhiliwa Bw Musyoka alipokuwa serikalini, lakini ujenzi ukalemazwa na maamuzi ya kisiasa yaliyofuata.

“Ni makosa kwa rais kwenda maeneo fulani leo na kudai analeta maendeleo, ilhali miradi hiyo ilizinduliwa 2013 na ikalemazwa,” alisema. “Wakenya si wajinga. Wanakumbuka nani alianzisha miradi hiyo na nani alichelewesha.”

Mbali na miundombinu, viongozi wa Wiper walipanua mjadala huo hadi masuala ya utawala na uadilifu. Seneta Abdalla alilinganisha kipindi cha Bw Musyoka serikalini na kile alichokitaja kama kukithiri kwa malalamishi ya wananchi chini ya utawala wa sasa.

“Kalonzo Musyoka aliondoka serikalini bila kashfa za ufisadi, bila utajiri usioelezeka na bila mizigo ya kimaadili inayokumba serikali ya sasa,” alisema. “Hauwezi kumhubiria maendeleo wakati huduma za afya zinaporomoka, elimu iko mashakani na gharama ya maisha inazidi kuwalemea wananchi.”

Mvutano huo unaashiria misimamo ya kisiasa mapema kuelekea 2027, huku Rais Ruto akijaribu kuwadhalilisha wapinzani wake na vyama vya upinzani vikichukulia mashambulizi hayo kama njia ya kuficha kutoridhika kwa wananchi na sera za serikali.

“Taifa hili halitajengwa kwa matusi na propaganda,” alisema Seneta Abdalla. “Uongozi ni kuhusu taasisi, uadilifu na huduma kwa wananchi, na hiyo ni rekodi ambayo Kalonzo Musyoka haogopi kuitetea.”