Habari

Siwezi kufanya kazi na Ruto, asisitiza Raila

January 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amesisitiza kuwa hawezi kamwe kushirikiana na Naibu Rais William Ruto kisiasa kutokana na tofauti za kimaadili baina yao.

“Maadili yangu ni imara na wazi kabisa. Tunatofautiana naye kimaadili,” akasema Bw Odinga kwenye mahojiano na NTV mnamo Jumapili usiku.

Alieleza kuwa japo hana tatizo endapo Wakenya watamchagua Dkt Ruto kuongoza nchi, hawezi kufanya kazi naye. Hii ni licha ya kuwa wawili hao walikuwa upande mmoja wakati wa uchaguzi mkuu wa 2007.

Matamshi hayo ya Bw Odinga ni kinaya kwa msimamo ambao amekuwa akitangaza kuwa dhamira kuu ya handisheki pamoja na Mpango wa Maridhiano (BBI) ni kuwaunganisha Wakenya wote na kuwa wako tayari kushirikisha kila mtu katika juhudi hizo.

Bw Odinga pia alionekana kumlaumu Dkt Ruto kama kizingiti kikubwa zaidi katika mpango wa Jopo la Maridhiano (BBI) akimtaja kuwa kigeugeu.

“Ni mtu anayeangalia jinsi mpango huu utamuathiri yeye binafsi ama maslahi yake huko mbele. Mnamo 2010 tulipokuwa tukipigania katiba mpya tulifanyishwa kibarua kigumu sana kuifanya ipitishwe. Sasa unapata baadhi ya waliokuwa wakiipinga wakisema haina tatizo na kuwa lengo la BBI ni kuundia watu fulani kazi. Hiyo ni ishara ya unafiki tulio nao hapa nchini,” akaeleza.

Dkt Ruto ni mmoja wa waliopinga katiba ya 2010 na sasa amekuwa akipinga baadhi ya mapendekezo ya BBI akidai inalenga kuongeza nyadhifa kuu serikalini.

Bw Odinga pia alimtaja Dkt Ruto kama muongo na kukanusha madai ya Naibu Rais kuwa alimtafuta wafanye maafikiano kabla ya kupatana na Rais Kenyatta.

“Nilishtuka niliposikia Ruto akisema kuwa nilimtafuta kwa ajili ya handisheki. Sikuwahi kuzungumza naye kwani hakukuwa na sababu yoyote ya kumtafuta,” akasema Raila.

Kwenye mahojiano hayo Bw Odinga pia alisema yeye si ‘Rais wa wananchi’ kama ambavyo amekuwa akiitwa na wafuasi wake tangu alipokula kiapo mbadala Januari 30, 2018.

Bw Odinga alisema sasa anamtambua Rais Kenyatta kama Rais wa Jamhuri ya Kenya, na kuwa wanashirikiana kukuza na kuunganisha taifa tangu handisheki iliyofuata kiapo hicho.

“Nilikana kiapo pindi tuliposalimiana na Rais. Hiyo ilikuwa ishara ya mwanzo mpya,” akasema.

Bw Odinga pia alikanusha kuwa yeye ni sehemu ya serikali ya Rais Kenyatta akisisitiza kuwa angali kiongozi wa upinzani. Hii ni licha ya kuwa amekuwa akiunga mkono sera na maamuzi ya serikali kinyume na awali ambapo alikuwa akiikosoa kwa hatua ambazo zilinyanyasa wananchi.

Bw Odinga pia amekuwa akishauriana na Rais kuhusu masuala tofauti ya kitaifa, suala ambalo linakinzana na madai yake kuwa angali katika upinzani.

Katika Bunge, wajumbe wa chama chake cha ODM wamekuwa wakipiga kura kila mara pamoja na wenzao wa upande wa Serikali.

Baadhi ya masuala mengine ambayo kiongozi huyo alizungumzia ni kuhusu uchaguzi wa uongozi ndani ya ODM ambao alisema umeahirishwa kutokana na kampeni za BBI.

“Hatutaki kuchanganya uchaguzi na suala la BBI. Tutakuwa na mkutano wa NEC ambao utaamua na kutangaza tarehe mpya,” akasema.

Alikiri kuwa vita vya kisiasa ndani ya chama hicho na madai ya ufisadi wakati wa uchaguzi vilisababisha kipoteze viti kadhaa katika Uchaguzi Mkuu wa 2017.

“Kumekuwa na visa vichache vya ufisadi, haswa maeneo ambapo uchaguzi wa mchujo wa ODM huwa ndio kama unaamua atakayeshinda Uchaguzi Mkuu. Ni hali ambayo ilituumiza kwani tulipoteza viti kadha maeneo ya Nairobi, Kisii, Magharibi na mengine nchini,” akasema.

Kuhusu Idara ya Mahakama, Bw Odinga aliilaumu kuwa haijajitolea kukabiliana na ufisadi, haswa miongoni mwa maafisa wake, na kuwa inalemaza vita dhidi ya ufisadi kwa kuua kesi.

“Wanajitetea kuwa ni upungufu wa pesa unaosababisha kesi kuchukua muda mrefu kortini. Lakini pia kuna majaji wafisadi na ambao bado idara hiyo inaendelea kuwapa mamlaka. Nimekuwa nikitetea Idara ya Mahakama lakini pia nayo inahitaji mageuzi ili kusikiza kesi kwa haraka na kuwafunga wafisadi,” akasema.