Sodoma na Gomora mitaani
Na MWANDISHI WETU
UOZO wa kimaadili katika jamii umefikia upeo baada ya kuongezeka kwa vilabu vinavyoonyesha wazi ngono kati ya wanaume na wanawake mitaani, Taifa Leo imefichua.
Vilabu hivyo ambavyo sasa vimeenea mitaani vimeibua wasiwasi hasa miongoni mwa wazazi wanaohofia kwamba huenda watoto wao wakapata mwanya wa kushuhudia maovu yanayoendelezwa humo.
Tofauti na vile vilabu ambavyo huwa na maonyesho ya wanawake au wanaume kuvua nguo wakisakata densi majukwaani almaarufu strip clubs, wasimamizi wa vilabu hivi hutumia maonyesho ya ngono kuvutia wateja.
Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini mitaa kama vile Rongai, Pipeline na Kayole ni kati ya maeneo yaliyo maarufu kwa vilabu vinavyoendeleza maonyesho hayo katika Kaunti ya Nairobi na viunga vyake.
Mbali na mitaani, vingine viko katikati ya jiji la Nairobi na katika mitaa ya kifahari.
Ijapokuwa ufichuzi kama huu umewahi kufanywa katika miaka iliyopita, kuendelezwa kwa biashara hii haramu na inayodhalilisha wanawake ni ishara wazi ya utepetevu kwa asasi za serikali zilizotwikwa jukumu la kuhakikisha kuwa kila biashara inayoendelezwa ni halali kwa msingi wa sheria za Kenya.
Baadhi ya wateja wa ‘burudani’ hii waliohojiwa na Taifa Leo ambao tumeamua kuwabana majina, walionyesha kutoshangazwa kamwe, wakisema ni jambo la kawaida ambalo wamekuwa wakifurahia kwa miaka kadhaa.
Ilifichuka kwamba katika vilabu kadhaa, maonyesho huwa ni ya ngono kati ya wanaume na wanawake lakini katika vilabu vingine, huwa ni wanawake wawili wanaotumia vidude mbalimbali kujifurahisha.
“Kutoka hapa tulipo sasa, naweza kukuonyesha vilabu vitatu aina hii ambavyo haviko mbali. Ni biashara… pia hao wanaotenda hayo mambo, ni riziki wanatafuta,” akasema mwanamume tuliyekutana naye mtaani Rongai.
Ilifichuka kuwa ingawa kuna vilabu ambavyo lazima mtu aonyeshe kitambulisho kabla ya kuingia, kuna kwingine ambako walinda-lango hawashughuliki kubainisha kama anayetaka kuingia amehitimu utu uzima au bado ni mtoto.
Vilevile, kuna vilabu ambako maonyesho hayo hufanywa katika vyumba maalumu ambako ni watu wachache tu huruhusiwa kuingia. Vyumba hivyo ni maarufu kama ‘VIP’, lakini vilabu vingine maonyesho ni wazi kwa yeyote aliyeingia.
Hili ndilo pengo ambalo linahofiwa huenda linawaachia watoto mwanya wa kushuhudia uozo huu.
Mbali na haya, kuna hofu pia kwamba huenda watoto wa kike wakavutiwa kuingilia mambo hayo wakiahidiwa malipo.
“Wenye vilabu wanataka faida na hii ni mbinu ya kuvutia wateja hasa wanaume. Maonyesho yanapoendelea, wao huendelea kuagiza vinywaji na hivyo kufaidisha kilabu usiku kucha,” akasema mkazi wa Nairobi anayefahamu mengi kuhusu shughuli hizo.
Ingawa mwandishi wetu hangeweza kubainisha wazi kiwango cha fedha ambacho wahusika hulipwa, duru zilisema wao hulipwa hadi Sh5,000 kwa usiku mmoja ikitegemea maelewano kati yao na wasimamizi wa vilabu.
Duru ziliongeza kwamba masuala ya kiafya hupewa uzito tu wakati wa ‘kuajiriwa’ lakini baadaye ni jukumu la mhusika mwenyewe kutafuta atakavyojilinda kutokana na magonjwa ya zinaa.