Sonko amenyana na serikali
Na RICHARD MUNGUTI
GAVANA wa Nairobi Mike Sonko ameelekeza mapambano yake na serikali kortini akilalamikia ubomoaji wa vibanda vya kunyunyizia watu sanitaiza wadumishe usafi na kupunguza hatari ya kuambukizana virusi vya corona.
Bw Sonko alisema alijenga vibanda hivyo vya sanitaiza kwa gharama ya Sh5 milioni jijini Nairobi.
Mahakama Kuu Jumanne ilitoa agizo la muda kwa Katibu wa Wizara ya Usalama, Dkt Karanja Kibicho, mawaziri Mutahi Kagwe (Afya), Fred Matiang’i (usalama) na maafisa wengine wakuu serikalini wasibomoe vibanda hivyo hadi kesi itakapokamilika.
Vibanda hivyo viliezekwa katika kituo cha kuabiri magari ya umma cha Kencom, nje ya Hospitali Kuu ya Kenyatta, na mitaa ya Buruburu, Korogocho, Mathare, Nyayo na Greenspan.
Jaji Korir aliratibisha kesi hiyo kuwa ya dharura na akamwagiza wakili wa gavana huyo, Bw Harrison Kinyanjui, awakabidhi washtakiwa nakala za kesi hiyo ili isikizwe Mei 12.
Wengine alioshtaki Sonko ni Kamishna wa Kaunti ya Nairobi, Bw Wilson Njenga, Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai na Mwanasheria Mkuu Kihara Kariuki.
“Washtakiwa walikaidi kifungu nambari 27 (4) cha Katiba kinachozuia ukandamizaji na ubaguzi wa aina yoyote ile ya wananchi kwa kubomoa vibanda hivyo mnamo Aprili 21, 2020,” akasema wakili Kinyanjui katika kesi hiyo.
Kando na hayo, gavana huyo amelalamika kwamba, maafisa wa serikali kuu wamevuruga mipango yake ya kusambaza misaada ya vyakula na mahitaji mengine ikiwemo barakoa kwa wenye mahitaji jijini.
Katika kesi yake, aliomba mahakama iamuru wakuu hao wa Serikali wasizuie utoaji wa vyakula vya misaada kwa familia zinazokumbwa na shida kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.
Alisema familia alizolenga ni za kutoka mitaa duni kama vile Kibera, Mathare na Huruma ambazo zilikuwa zinawasilishiwa misaada kupitia kwa kikundi chake cha uhisani cha Sonko Rescue Team.
Wakili huyo alisema hatua ya kuzuia misaada kufikia wenye mahitaji ni ubaguzi wa hali ya juu kwa wakazi wa Nairobi wasio na uwezo wa kujikimu kimaisha.
Mahakama imeelezwa kuwa, Wizara ya Afya ama shirika lolote lile la Serikali hazikufadhili usambazaji wa barakoa za bure kwa wananchi wasio na uwezo wa kujinunulia, na hivyo basi ni makosa kuzuia wafadhili kuzisambaza.
Katika malalamishi yake, Bw Kinyanjui alisema inasikitisha sana kuona misaada ya kundi hilo la Sonko ikizimwa ilhali mawaziri husika na maafisa wakuu serikalini hawakuzima usambazaji wa misaada ya wahisani wengine kama vile Mama Ngina Kenyatta, aliyekuwa makamu wa Rais Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Alisema misaada pia huendelea kutolewa na mashirika mbalimbali ya watu binafsi kama vile muungano wa hoteli za Sarova kwa maafisa wa afya wanaopambana na walioathiriwa na ugonjwa huu wa Covid-19 katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.