Habari

Sonko azongwa

December 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko jana Alhamisi alikabiliwa na wakati mgumu kujitetea mbele ya maseneta dhidi ya mashtaka ya kumtimua afisini.

Mara kadha, Bw Sonko alikwepa kujibu maswali aliyoulizwa na mawakili wa bunge la kaunti akiwaelekeza kwa mawakili wake wakiongozwa na Harrison Kinyanjui.

Isitoshe, nyakati fulani gavana huyo alipandwa na hasira na kuwarushia maneno makali mawakili wa bunge la kaunti ya Nairobi akidai wanatumiwa kudhalilisha hadhi yake kama gavana “na baba mzazi.”

Licha ya gavana kukana madai kwenye hoja hiyo kwamba alitumia Sh297 milioni za basari ya masomo kuwalipa mawakili wake na kampuni zilizopewa zabuni za uzoaji taka, wakili wa bunge la kaunti ya Nairobi, Ndegwa Njiru alitoa stakabadhi zilizoonyesha malipo hayo yalifanywa.

Kulingana na stakabadhi hizo, wakili Kwanga Mboya alilipwa Sh80 milioni huku wakili Cecil Miller akilipwa Sh83.7 milioni. Wawili hawa ni miongoni mwa kundi la mawakili walioorodheshwa kumtetea Gavana Sonko mbele ya maseneta.

“Ningependa kuthibitishia bunge hilo la Seneti kwamba hizi ndizo fedha ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya basari za watoto kutoka kutoka familia maskini katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020” akasema Bw Njiru.

Hata hivyo, Bw Sonko alisema kuwa wakili Mboya alilipwa Sh80 milioni kufuatia amri ya Jaji wa Mahakama Kuu, John Mativo.

“Ningependa kuambia Seneti kuwa Sh297 milioni za basari hazikutolewa baada ya sakata ya ufisadi kufichuliwa katika mpango huo wa kuwasaidia watoto kutoka familia maskini. Sh80 milioni ambazo zililipwa Wakili Mboya hazikutolewa kutoka kwa mfuko wa basari na zililipwa kutokana na amri ya mahakama,” gavana huyo akasema.

Bw Sonko alidai taasisi ya kielimu kwa jina Kobudho Educational Centre kama ambayo mfadhili wa hoja hiyo Diwani Michael Ogada na madiwani wenzake walitumia kufyonza fedha za mpango wa basari.

“Wakurugenzi wa taasisi hii ya Kobudho ni wake na washirika wa madiwani wa kaunti ya Nairobi akiwemo mdhamini wa hoja hii Bw Ogada. Nilipoingia mamlakani nilisimamisha utoaji wa fedha za basari na kupiga ripoti kwa maafisa wa Idara ya Upelekezi wa Jina (DCI) ambao waliwakamata wahusika,” akaeleza.

Kuhusu madai kuwa bintiye Saumu Mbuvi alitumia mamilioni fedha za kaunti ya Nairobi kama ziara ya anasa jijini New York Amerika, gavana Sonko alikana madai hayo akisema ziara hiyo iligharimu Sh4.3 milioni pekee.

Bw Sonko alisema ziara ya bintiye, ambaye aliandamana na mkewe, ilidhaminiwa na Serikali ya Kitaifa na ikaidhinishwa na Ikulu ya Rais.

“Ni kweli kwamba binti yangu na mke wangu walienda Amerika. Lakini walikuwa katika ujumbe wa serikali kuu ambayo ndio ilifadhili safari yao kwa kima cha Sh4.3 milioni wala sio Sh800 milioni wanavyodai wadhamini wa hoja yenye nia ya kuniharibia jina,” akasema na kutoa barua kutoka mkuu wa utumishi wa umma ikiidhinisha ziara hiyo.

MKEWE

Hata hivyo, Gavana Sonko alikubali kuwa mkewe, Primrose Mbuvi, alipokea marupurupu ya matumizi kutoka kwa Kaunti ya Nairobi lakini kupitia mwanamke aliyemrejelea kwa jina moja kama Josphine

Lakini hakufafanua uhusiano ulioko kati ya Bi Josphine, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni kwa jina Premier na mke wake.

Kuhusu madai ya sakata ya ufisadi iliyozonga mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo ya Dandaro, Bw Sonko alijitetea vikali kwa kukana kuwa wanakandarasi walilipwa Sh196 milioni kinyume cha sheria.

“Kiasi cha fedha zilizolipwa wanakandarasi hazikuzidi Sh100 milioni. Hayo madai ya Diwani Ogada na wenzake ni ya uwongo,” Sonko akasema.

Akaongeza: “Nataka bunge hili la Seneti lifahamu pia kwamba suala hili lingali linachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) baada ya mradi huo kusitishwa kutokana na madai ya madai ya ufisadi.

Gavana Sonko pia alisema kuwa ujenzi wa uwanja huo wa michezo haujakamilishwa kutokana na kesi kadha zilizowasilishwa kortini.

Kuhusu madai kuwa alidinda kuidhinisha bajeti iliyoitengea Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) ya Sh27.9 bilioni, Bw Sonko alisema alifanya hivyo kwa sababu mahakama ilitoa uamuzi kuwa asasi hiyo ilibuniwa kinyume cha sheria.

“Isitoshe, mahakama zilikuwa zimesimamisha kupitishwa kwa bajeti hiyo. Kwa hivyo, singeingilia suala ambalo lilikuwa linashughulikiwa na korti,” akasema.