Habari

Sonko kuondoa kesi dhidi ya NMS

August 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi, Mike Sonko alitangaza Alhamisi kuwa ataondoa kesi zote dhidi ya Idara ya Huduma za Nairobi (NMS).

Hatua yake ilijiri siku moja baada ya kuridhiana na Mkurugenzi wa shirika hilo Meja Jenerali Mohammed Badi kutokana na shinikizo za Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Sonko alisema ameamua kuweka kando tofauti zake na Bw Badi kwa manufaa ya wakazi wa Nairobi.

Mnamo Jumatano, Rais Kenyatta alimuonya gavana huyo kuwa hatavumilia siasa duni jijini Nairobi.

Akiongea katika jumba la mikutano la Kenyatta (KICC) baada ya kutoa hati miliki kwa wakazi, Rais Kenyatta alisema hatakubali siasa kuyumbisha mipango yake ya kustawisha jiji la Nairobi.

“Kuanzia sasa hatutakuwa na kesi yoyote kortini tena. Tutaketi na Bw Badi na kusuluhisha tofauti zote tulizokuwa nazo kuonyesha nia njema. Tutaondoa kesi zote na kusahau ya zamani,” alisema Bw Sonko.

Gavana Sonko alisema hayo alipoandamana na madiwani sita kukagua miradi ya maendeleo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru.

Ulainishaji wa mambo

Alikiri kwamba kuna masuala kadhaa yasiyomfurahisha katika utekelezaji wa mkataba wa kuhamisha majukumu kwa serikali ya kitaifa aliotia sahihi Februari 25, 2020, katika Ikulu ya Nairobi, lakini akasema ataketi na Bw Badi kulainisha mambo kwa amani.

Kuna kesi kortini inayopinga hatua ya NMS ya kuteua bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya maji ya Nairobi.

Katika kesi nyingine iliyowasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtatah, mahakama ilipatia NMS na serikali ya kaunti hadi Juni kuhalalisha mkataba wao.