Sonko kuongoza wakazi wa Kibra kumjulia hali mbunge Ken Okoth
Na CHARLES WASONGA
GAVANA wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko ameahidi kuwadhamini wakazi wachache wa eneobunge la Kibra kwenda kumjulia hali mbunge wao, Ken Okoth, anayepokea matibabu nchini Ufaransa.
Mbunge huyo anaugua kansa ya utumbo (colorectal cancer) ambaye awali aliungana kwamba iligunduliwa kuchelewa.
Kwenye ujumbe aliouweka kwenye ukurasa wake wa Facebook, Gavana Sonko aliwataka wakazi wa Nairobi kumwombea Bw Okoth ili apate afueni.
“Nitajitolea pia kudhamini na kuongoza ujumbe wa mapasta, maimamu, na wakazi wachache wa Kibra kumtembelea nchini Ufaransa kumwombea mbunge wetu. Afueni ndugu. Endelea kumwamini Mungu,” Sonko akasema.
Sonko aliongeza kuwa wakati umetimu kwa taifa hili kusaka suluhu la kudumu la kupambana na kansa.
“Kansa inatuathiri zaidi. Jambo muhimu katika kukabiliana na ugonjwa ni kutopoteza matumaini. Hata hivyo, kama taifa tunapawa kupata njia bora ya kukabili ugonjwa huu hatari,” akaongeza.
Awali, Bw Okoth alifichua kuwa amepitia hali ngumu kupambana na kansa lakini alielezea matumaini kuwa atashinda.
Unyanyapaa unaokuandama inapogunduliwa kuwa unaugua kansa ni mkubwa. Kansa hubadili kabisa maisha ya mwanadamu,” akasema mwezi wa Mei alipotembelewa na baadhi ya wabunge wakiongozwa na Mbunge wa Aldas Aden Keynan.