Habari

Sonko kupokea kiwango cha juu cha fedha huku Fahim Twaha akipokea kidogo

September 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KAUNTI za Nairobi, Turkana, Nakuru, Kilifi, Kakamega na Mandera ni miongoni mwa zile ambazo zitapata sehemu kubwa ya mgao wa Sh316.5 bilioni ambazo zimetumwa kwa serikali 47 za kaunti katika mwaka huu wa kifedha wa 2019/2020.

Kulingana na Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARB) wa 2019 uliopitishwa Jumatano katika bunge la kitaifa, Kaunti ya Nairobi ndio itapokea kiasi kikubwa zaidi cha Sh15.91 bilioni.

Inafuatwa na Kaunti ya Turkana ambayo itapata Sh10.53 bilioni huku Kaunti ya Nakuru ikipokea Sh10.47 bilioni.

Nazo kaunti za Kilifi, Kakamega na Mandera zitagawiwa Sh10.44, Sh10.41 na Sh10.22,mtawalia. Kaunti ya Kiambu nayo imepokea Sh9.43 bilioni.

Kwa upande mwingine kaunti za Lamu, Tharaka Nithi, Elgeyo Marakwet, Laikipia, Isiolo na Kirinyaga ni miongoni mwa zile ambazo zitapata mgao mdogo zaidi ikilinganishwa na zingine.

Kaunti ya Lamu inayoongozwa na Gavana Fahim Twaha itapokea Sh2.59 bilioni huku Tharaka Nithi yake Muthomi Njuki ikipata Sh3.92 bilioni za kufadhili shughuli zake na kufadhili miradi ya maendeleo.

Kaunti ya Elgeyo Marakwet itapata Sh3.86 bilioni, Laikipia (Sh4.17 bilioni), Isiolo (Sh4.24 bilioni) huku Kirinyaga ikipata Sh4.24 bilioni.

Kulingana na mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na Bajeti Bw Mohamed M. Mahamud, idadi ya watu, kiwango cha umaskini na ukubwa wa kaunti ndivyo vigezo vikuu vilivyotumiwa kukadiria kiasi cha mgao wa fedha katika kila kaunti.

“Hii ndio maana kaunti kama Nairobi, Nakuru, Kakamega, na Kiambu zimepata mgao wa juu kwa misingi ya kuwa na idadi kubwa ya watu. Na kwa upande mwingine kaunti za Turkana, Kilifi na Mandera zimefaidi kwa mgao wa juu kwa sababu ni maeneo kame yenye kiwango cha juu cha umasikini,” anasema anapotoa maelezo kuhusu malengo ya mswada huo.

Mswada huu ulipitishwa na Seneti Jumanne katika vikao vyake vinavyoendeshwa katika Kaunti ya Kitui.

Unatarajiwa kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta leo ili kutoa nafasi kwa usambazaji wa Sh50 bilioni ambazo zilitolewa Jumanne na Hazina ya Kitaifa.

Hii ni baada ya Rais kutia saini mswada wa ugavi wa fedha kati ya serikali kuu na zile za kaunti ambao ulikuwa umekwama kwa miezi miwili.

Kukwama kulisababishwa na mvutano kati ya maseneta na wabunge kuhusu kiasi cha fedha ambazo zinafaa kutengewa serikali za kaunti katika mwaka huu wa kifedha.

Hata hivyo, muafaka ulipatikana majuzi pale maseneta walipokubaliana na msimamo wa wabunge kwamba kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni.

Awali, maseneta walipendekeza serikali hizo 47 zitengewe Sh335 bilioni.

Mnamo Jumanne kaimu Waziri wa Fedha Ukur Yatani alisema baada ya Rais Kenyatta kutia saini mswada wa CARB ljumaa, serikali za kaunti zitaanza kupokea sehemu ya mgao wao, wa miezi ya Julai na Agosti, kuanzia kesho Alhamisi.

Kutolewa kwa fedha hizo ni afueni kubwa kwa kaunti hizo ambazo zimekuwa zikikumbwa na uhaba wa fedha kiasi cha kushindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi.