Sonko ndiye alijichimbia shimo lake – Wataalamu
Na CHARLES WASONGA
ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko alianza kujiangusha mwenyewe mwezi mmoja baada ya kubuniwa kwa Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) alipoanza kuipiga vita, wadadisi wanasema.
Hii ni licha ya kwamba alitia saini mkataba uliohamisha majukumu manne makuu ya serikali yake hadi serikali kuu na kuwekwa chini ya usimamizi wa asasi hiyo inayoongozwa na Meja Jenerali Mohamed Badi.
Majukumu hayo ni Afya, Uchukuzi, Mipango na Ujenzi na usimamizi wa idara za usafi na maji.
Kimsingi, Sonko aliamua kuhujumu utendakazi wa NMS, akidai sio halali na kwamba ilitwaa majukumu mengine ambayo hayakuwa yamehamishwa hadi serikali kuu kulingana na mkataba huo uliotiwa saini mbele ya Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi mnamo Februari 25, 2020.
Kilele cha ukaidi wake kilijiri Oktoba 2020 alipodinda kutia saini bajeti ya serikali ya Nairobi iliyoitengea NMS Sh27.7 bilioni za kufadhili miradi yake.
Hii ni licha ya Rais Kenyatta kila mara kumtaka Bw Sonko kuunga mkono NMS na kufanya kazi na Meja Badi “kwa manufaa ya wakazi wa Nairobi.”
Kulingana na machanganuzi wa masuala ya siasa Javas Bigambo, Bw Sonko alifeli kung’amua hatari iliyokuwa ikimkodolea macho kutokana na hatua yake ya kukaidi ushauri wa Rais Kenyatta.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba Rais Kenya na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ndio walimnusuru mapema mwaka huu madiwani walipotaka kumbadua.
“Hekima ingemwongoza Sonko kutambua kuwa ni Rais aliyeshawishi kuondolewa kwa hoja ya kwanza ya kumtimua afisini Januari 2020 na kuamua kubuni NMS kuendesha majukumu muhimu ya kaunti. Hii ni baada ya Jaji wa Mahakama Kuu Mumbi Ngugi kuamua asiingie afisini hadi kesi za ufisadi zilizokuwa zikimkabili zisikiLIzwe na kuamuliwa,” anasema Bigambo.
Rais Kenyatta amekuwa akisifia utendakazi wa NMS, akisema umechangiwa na hali kwamba asasi hiyo inasimamiwa na maafisa wa kijeshi wenye hulka ya kuongozwa na maadili na nidhamu katika utendakazi wao.
Akiongea juzi katika ukumbi wa Bomas alipohudhuria hafla ya vijana, Rais Kenyatta alisema NMS imebadili sura ya Nairobi na kuimarisha utoaji huduma kwa wakazi.
“Ndani ya miezi tisa pekee tangu kubuniwa kwa NMS, idara hii imeweza kujenga upya barabara ya umbali wa kilomita 4,000 katika jiji la Nairobi. Kwa hivyo, ningependa kuwaambia wale ambao wanapinga utendakazi wa wanajeshi kukubali kuwa wao wenyewe walishindwa na kazi kama hii,” akasema Rais, huku akionenakana kumrejelea Bw Sonko.
Bw Sonko pia anasemekana kujiletea taabu kwa kufeli kupalilia uhusiano wa karibu na madiwani wa kaunti hiyo tangu alipoingia mamlakani miaka mitatu iliyopita.
Chini ya utawala wake, madiwani walikuwa wamegawanyika katika mirengo miwili, wanaomunga mkono na wale wanaompinga.