Suluhu agonganisha maafisa wa Kenya kuhusu kufurushwa kwa wanaharakati
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameibua mjadala nchini Kenya, kufuatia onyo lake kwa wanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya na Uganda waliotimuliwa Tanzania kwa kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu.
Huku waliotimuliwa wakiapa kushtaki serikali ya Tanzania, Waziri wa mashauri ya kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi ameonekana kugongana na katibu wake Korir Arap Sing’oei. Huku Mudavadi akiunga Rais Suluhu Dkt Sing’oei alihimiza Tanzania kuheshimu misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza kwenye Citizen TV usiku wa Jumanne, Mudavadi alionekana kuunga mkono kauli za Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kile alichokitaja kuwa ‘kuingilia masuala ya ndani’ ya Tanzania na kuonyesha wasiwasi wake kuhusu ‘ukosefu wa maadili’ wa Wakenya katika mienendo yao ya hivi karibuni.
Tofauti na Mudavadi,Katibu Sing’oei, aliitaka serikali ya Tanzania kuwaachilia mara moja Jaji Mkuu Mstaafu Willy Mutunga na ujumbe wake,
Sing’oei alisisitiza kuwa kuzuiliwa kwa ujumbe huo wa Kenya kulikiuka misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo inahimiza uhuru wa kusafiri, na ushirikiano kati ya nchi wanachama.
“Tunasihi serikali ya Tanzania kuachilia aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya na ujumbe wake, kwa mujibu wa taratibu na misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Sing’Oei.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alishangaa jinsi waziri Mudavadi anaweza kuunga kutimuliwa kwa Wakenya kutoka nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Bw Sifuna alitilia shaka msimamo wa Mudavadi kuhusu haki za Wakenya nje ya nchi.
Kulingana na Sifuna, ni jambo la kushangaza kwa Waziri huyo kutoa matamshi hayo ilhali Wakenya, akiwemo mwanaharakati na mwandishi wa habari Boniface Mwangi, aliokamatwa nchini Tanzania hajulikani aliko.
‘Kwa Waziri wetu wa Masuala ya Nje kuunga mkono Tanzania kuhusu kufukuzwa kwa Wakenya ni jambo la ajabu. Ni nani aliwaweka hawa watu madarakani? Hawana maana kabisa,’ Sifuna alilalamika.
Kulingana na Mudavadi, Rais Suluhu huenda alizungumza kwa kuzingatia tabia za baadhi ya Wakenya hivi karibuni.
‘Sitapinga kauli hiyo (ya Suluhu) kwa sababu nafikiri kuna ukweli fulani. Tuwe wakweli. Kiwango cha lugha chafu na matusi tunayoona Kenya, ingawa tuna uhuru wa kujieleza, wakati mwingine kinavuka mipaka. Anasema watu wamekuwa wakivuka mipaka katika kauli zao, jambo ambalo ni la kweli,’ alisema Mudavadi.
Mnamo Jumapili, kiongozi wa chama cha Peoples Liberation Party, Martha Karua, alizuiwa kuingia Tanzania akiandamana na watetezi wa haki za binadamu na wanasheria, Lynn Ngugi na Gloria Kimani.
Karua alisema alifukuzwa nchini humo baada ya kuzuiliwa kwa muda mrefu katika uwanja huo wa ndege.
Siku moja baadaye, wanaharakati wengine watatu wa Kenya, akiwemo Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga, walikamatwa.
Mutunga, aliyekuwa akisafiri na mwanaharakati Hanifa Adan pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa VOCAL Africa, Hussein Khalid, alikamatwa walipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere baaada ya kurejeshwa Kenya.
Jana, Bw Khalid alisema mwanaharakati maarufu Boniface Mwangi kutoka Kenya, pamoja na mwandishi na wakili kutoka Uganda, Agatha Atuhaire, waliokamatwa na maafisa wa Tanzania hawajulikani waliko.
“Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire hawajulikani walipo. Baada ya kutumia njia zote jijini Dar es Salaam, hatujaweza kuthibitisha waliko. Tumekagua mashirika yote ya ndege na tumefuatilia kwa wanasheria nchini Tanzania, lakini bado hawajulikani waliko,”alisema Khalid.
“Tumejaribu kuwatafuta pamoja na watetezi wa haki za binadamu na wanasheria nchini Tanzania bila mafanikio. Ijulikane kuwa Wakenya watamlaumu Rais Suluhu Hassan binafsi endapo chochote kitatokea kwa wawili hao.”
Mnamo Jumanne, Boniface Mwabukusi, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alitangaza kuwa serikali ya Tanzania ilimtumua Mwangi na Atuhaire.
Katika taarifa yake, Mwabukusi alisema wawili hao walifukuzwa chini ya usimamizi wa maafisa wa uhamiaji wa Tanzania.
“Boniface Mwangi, mwandishi wa habari na mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya, na Bi Agatha Atuhaire, mwandishi wa habari na wakili kutoka Uganda, ambao walikuwa wakizuiliwa katika Kituo cha Polisi jijini Dar es Salaam, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tangu Mei 19 2025, wamefukuzwa na kurejeshwa katika nchi zao,” alisema Mwabukusi.
Mwangi, aliyewasili Tanzania Jumapili kuhudhuria kesi ya kiongozi wa upinzani Tundu Lissu iliyopangwa siku iliyofuata, alikamatwa siku ya Jumatatu, Mei 19, baada ya serikali ya Tanzania kudai aliingia nchini humo kwa njia isiyo halali.