Tamko la 'Washenzi' lilivyowakera wapigakura wa Mlima Kenya
JOSEPH OPENDA, BENSON MATHEKA Na CHARLES WASONGA
TAMKO la Rais Uhuru Kenyatta la kuwaita “washenzi” wale wanaomkosoa kwa madai ya kupuuza eneo la Mlima Kenya kimaendeleo, limeibua shutuma kali na tafsiri kuwa alilenga jamii yote ya eneo hilo kwenye kauli yake.
Wakazi wengi wa eneo la Mlima Kenya walichukulia kauli ya rais kama matusi kwa wote waliompigia kura huku wakieleza hasira zao kwenye mitandao na kupiga simu kuchangia mijadala kwenye vituo vya redio na runinga wakieleza kukasirishwa kwao na rais.
Hii ni licha ya kuwa matamshi ya rais mnamo Jumatatu yalionekana kulenga viongozi pekee waliomkosoa na wala sio jamii nzima ya Mlima Kenya.
Wakazi wengi wa eneo hilo jana walitaja kauli ya rais kama madharau makubwa kwao licha ya kumpigia kura kwa wingi tangu 2013.
Kauli hiyo ilikuwa mada kuu kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari tangu Jumatatu wakati Rais Kenyatta alipoitoa akiwa Mombasa. Kilele chake kilikuwa ni maandamano yaliyoongozwa na Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri kulalamikia matamshi hayo.
Mnamo Jumatatu, Rais Kenyatta aliwataja kama “washenzi” wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakidai kuwa serikali yake imetenga eneo hilo kimaendeleo.
“Wajibu wangu kama Rais ni kuhakikisha kuwa maendeleo yanasambazwa katika pembe zote nchini. Kuanzia sasa nitazunguka kuanza Kisumu hadi Mombasa, Namanga hadi Lodwar kuzindua miradi ya maendeleo. Hizi siasa za kutaka maendeleo yakite katika eneo ambako kiongozi anatoka pekee sharti zikome,” akasema akiwa Mombasa.
Malumbano makali yalizuka mitandaoni jana huku baadhi kutoka nje ya Mlima Kenya wakiandika: “Mlipiga kura na sisi twavuna.”
Mjini Nakuru, Bw Ngunjiri aliongoza kundi la vijana kwenye barabara ya Kenyatta waliokuwa wakiiba “mimi ni mshenzi” kabla ya kuzindua vuguvugu la ‘Washenzi Movement’.
Hapo jana jioni Bw Ngunjiri alikuwa akisakwa na polisi kufuatia maandamano hayo.
Umaskini kuongezeka
Kulingana na mbunge huyo ambaye Jumapili alikashifu vikali uongozi wa Rais Kenyatta akisema umeongeza umasikini, lengo la vuguvugu hilo ni kutuma ujumbe kwa rais kwamba waliompigia kura kwa wingi wanahisi amewapuuza: “Tumeanzisha vuguvugu hili kuonyesha rais kwamba wapigakura 8.2 milioni wa eneo la Mlima Kenya sio wajinga. Watu waliompigia kura wamesikitishwa na mwelekeo anaochukua,” alisema Bw Ngunjiri.
Matamshi ya Rais Kenyatta yalijiri siku moja baada ya Bw Ngunjiri kumuunga mkono Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria katika kulaumu serikali kwa madai ya kupuuza eneo la Mlima Kenya kimaendeleo.
Kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance, Ekuro Aukot kwa upande wake alimtaka Rais Kenyatta kuwa mstari wa mbele kupalilia maridhiano ya kisiasa kwa kukoma kutumia lugha ya matusi dhidi ya wanasiasa ambao wanakosoa uongozi wake.
“Yeye ni kiongozi wa taifa na anapaswa kuonyesha uvumilivu. Hafai kuwazomea viongozi wengine hadharani kwa maneno makali ambayo siwezi hata kuyatamka hapa. Rais Kenyatta pia akome kuwaambia Wakenya waachane naye. Waachane naye vipi ilhali yeye ni rais wao?” akasema Bw Aukot.
Seneta wa Kiambu, Kimani Wamatangi naye alikiri kuwa eneo la Mlima Kenya limekosa miradi mikubwa ya maendeleo, lakini akakosoa mbinu ya kumshambulia rais katika kuwasilisha ujumbe huo.
Bw Wamatangi alisema tatizo kuu ni mfumo wa ugawaji wa raslimali za kitaifa, suala ambalo linapasa kuangaziwa zaidi: “Watu wa Mlima Kenya wanamlilia rais kwa sababu anatoka eneo hilo. Akiondoka madarakani 2022 watamlilia nani? Suluhisho ni kurekebisha mfumo wa kugawa raslimali za kitaifa ili kutendea haki kaunti zote.”
Naye mwenyekiti wa wabunge wa eneo la Mlima Kenya, Cecily Mbarire aliwataka wenzake na wakazi wa eneo hilo kumheshimu Rais Kenyatta akisema ana jukumu la kuhudumia Wakenya wote.