'Tangatanga' wageuka tena, wasema watahudhuria mikutano ya BBI iliyoandaliwa na kundi la Rais na Raila
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wa ‘Tangatanga’ sasa wamefutilia mbali mikutano yao binafsi ya uhamasisho kuhusu ripoti ya BBI na kutangaza kuwa sasa watashiriki mikutano iliyoandaliwa na viongozi wanaoegemea mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika seneti Kipchumba Murkomen, wabunge hao tisa wamesema watahudhuria mkutano wa Jumamosi mjini Kitui utakaongozwa na Bw Odinga.
“Tofauti na kauli yetu katika mkutano wa Naivasha na kulingana na nia yetu ya kuvumisha masuala yanayowahusu raia, kwa niaba ya wenzetu tumefutilia mbali mikutano tulioratibu kuanzia Februari 8. Tutahudhuria wa kesho (Kitui) na mingine ambayo imeratibiwa,” Bw Murkomen amesema kwenye kikao na wanahabari Ijumaa katika majengo ya bunge.
Aliandamana na wenzake; Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Moses Lessonet (Eldama Ravine), Moses Letoimaga (Samburu Kaskazini), Korei Lemeiy (Narok Kusini) na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot.
Viongozi hao pia wamewataka wanachama wa kamati ya Maridhiano inayoongozwa na Seneta Yusuf Haji kutuma maafisa wake katika mikutano hiyo ya uhamasisho ili wakusanya maoni na mapendekezo ya wananchi.