HabariSiasa

Tangatanga walaani serikali kufungia Ruto nje ya makazi

January 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WANDANI wa Naibu wa Rais William Ruto almaarufu Tangatanga Jumapili walidai kuwa kuna maafisa fulani katika Afisi ya Rais ambao wanaendeleza kampeni za kumhujumu.

Hii ni kufuatia habari iliyochapishwa kwenye gazeti la Sunday Nation,  Januari 12, kwamba Dkt Ruto alizuiwa kuingia katika makazi yake rasmi mjini Mombasa.

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria walidai kuwa maafisa hao ambao hawakuwataja ndio pia wamekuwa wakiwahangaisha viongozi wanaounga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

“Kuna watu fulani serikalini wanajidanganya kwa kumkosea heshima Naibu Rais William Ruto na sisi kama wafuasi wake. Lakini nataka kuwaambia kwamba hawatafaulu,” akasema Bw Kuria.

Mbunge huyo aliachiliwa huru Jumamosi kwa bondi ya polisi baada ya kushikwa kwa tuhuma za kumpiga mwanahabari mmoja wa kike katika studio za Shirika la Habari la Royal Media, mnamo Desemba 8, 2019.

Huku akilaani kitendo hicho, Seneta Cheruiyot alilinganisha yaliyompata Dkt Ruto na Wakenya wa kawaida ambao nyakati zingine hupata wamefungiwa milango ya nyumba zao kwa kutolipa kodi.

“Kama mahasla wa kawaida Naibu Rais alirejeaa kutoka Krismasi na kupata kufuli langoni… shida za kawaida mwezi wa Januari. Tunawajua waliotekeleza kitendo hicho lakini najua watafeli. Kaa ngumu Dkt Ruto,” Bw Cheruiyot akasema katika ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter.

Makazi rasmi ya Naibu Rais yalifanyiwa ukarabati kwa gharama ya Sh152.4 milioni mnamo 2018 kwani zamani ilikuwa makazi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani chini ya utawala wa zamani wa mikoa.

Ilitarajiwa kuwa akizuru Pwani kwa shughuli za kikazi, Dkt Ruto angeishi hapo badala ya katika hoteli za kibinafsi.

Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa katika “Sunday Nation”, majuzi Dkt Ruto alilazimika kulala katika hoteli ya English Point Marina baada ya kufika katika makazi yake rasmi na kuwapa wafanyakazi wakipakia nguo zake, kufuatia agizo “kutoka juu”.

Lakini akiongea na gazeti hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Afisi ya Naibu Rais Emmanuel Tallam alidai hakuwa na habari kuhusu yaliyomfika Dkt Ruto Mombasa.

“Sifahamu chochote kuhusu habari hizo. Nation ndio wanafahamu walikopata ripoti hiyo,” akasema huku akiongeza kuwa Dkt Ruto hulala katika Mkahawa wa Englisha Point Marina anapozuru Mombasa.