HabariSiasa

Tangatanga yatumia sakata ya fedha za corona kutakasa Ruto

August 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

MADAI kuhusu wizi wa mamilioni ya fedha zilizotengwa kukabiliana na janga la virusi vya corona yamegeuka baraka kwa Naibu wa Rais William Ruto huku wandani wake wakiyatumia kumtakasa.

Kulingana na wanasiasa wanaounga mkono Dkt Ruto, maarufu Tangatanga, sakata hiyo ya wizi wa fedha za corona, imedhihirisha kuwa madai ya ufisadi ambayo Naibu wa Rais amekuwa akilimbikiziwa ni porojo tu.

Rais Kenyatta amemtenga naibu wake Dkt Ruto katika juhudi za kukabiliana na janga la virusi vya corona. Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na mwenzake wa Usalama Fred Matiang’i, ndio wamekuwa wakiongoza juhudi za kupambana na maradhi ya corona.

Naibu wa Rais Ruto hajakuwa akialikwa kuhudhuria vikao ambapo Rais Kenyatta amekuwa akihutubia taifa kila mwezi. Dkt Ruto, hata hivyo, amekuwa akishirikishwa kwenye mikutano ya Rais Kenyatta na magavana kujadili maandalizi yanayofaa kuwekwa na kaunti ili kukabiliana na idadi kubwa ya wagonjwa wa virusi vya corona.

Wanasiasa wa Tangatanga wakiongozwa na mbunge wa Soy Caleb Kositany, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, sasa wanataka wizara ya Afya kuelezea namna imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha zilizotengwa kupambana na virusi vya corona.

Hii ni baada ya ripoti kufichua kuwa kandarasi za kuleta vifaa vya kukinga wahudumu wa afya dhidi ya kupatwa na virusi vya corona, maarufu PPEs, zilipewa jamaa na marafiki wa viongozi wakuu serikalini na chama cha Jubilee.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, wafanyabiashara hao walaghai waliuzia serikali vifaa hivyo kwa bei maradufu ikilinganishwa na bei ya sokoni.

Watu wenye ushawishi serikalini, kulingana na ripoti, waliiba hata msaada wa kupima virusi vya corona uliotolewa na bwanyenye wa China, Jack Ma.

Bw Kositany alidai kuwa wizara ya Afya imetumia mamilioni ya fedha kupatia Idara ya Ujasusi (NIS) kutafuta watu wanaotangamana na waathiriwa wa virusi vya corona.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, jana aliambia Taifa Jumapili kuwa sakata hiyo ya wizi wa fedha za corona, imemwondolea lawama Dkt Ruto ambaye amekuwa ‘akipakwa tope’ na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini kwamba ni mfisadi.

Dkt Ruto amekuwa akisema kuwa madai ya ufisadi ambayo amekuwa akihusishwa nayo hayana msingi na yanalenga kumchafulia jina ili kuzima azma yake ya kuwania urais 2022.

“Ruto hajahusishwa katika masuala ya kupambana na janga la virusi vya corona, sasa tunataka tuambiwe aliyeiba Sh30 milioni za corona. Wakenya sasa wanajua mwizi ni nani,” anasema Bw Sudi.

Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye ni mmoja wa nguzo muhimu za Dkt Ruto katika eneo la Magharibi, sasa anataka Naibu wa Rais Ruto kupewa usimamizi wa Kamati ya Kitaifa ya Kukabiliana na janga la virusi vya corona.

“Mheshimiwa Rais, ili kuboresha utendakazi wa kamati ya kukabiliana na virusi vya corona, Naibu wa Rais anafaa kupewa usimamizi wake,” akasema Bw Khalwale kupitia akaunti yake ya Twitter.

Mkurugenzi wa shirika la kijamii Internnational Centre for Policy and Conflict (ICPC) Ndung’u Wainaina, anataka Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kuwajibika kwa ujiuzulu kufuatia madai ya ubadhirifu wa fedha za kupambana na virusi vya corona.

“Inashangaza kwamba serikali inatuma wakaguzi wa hesabu katika kaunti kuchunguza namna zimetumia mamilioni ya fedha zilizotengewa vita dhidi ya corona. Ukweli ni kwamba, wizara ya Afya ndiyo inafaa kuchunguzwa kwanza,”anasema Bw Wainaina.

Naye wakili Ahamednasir Abdullahi, anamtaka Rais Kenyatta kujitokeza na kuwaadhibu waliohusika na ubadhirifu wa fedha za corona. Aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando, anasema kuwa sakata hiyo ya fedha za corona imemtakasa Dkt Ruto.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukiambiwa kwamba Naibu wa Rais ni fisadi lakini sasa madai hayo yameanza kukosa mashiko,” akasema Bw Kabando ambaye hivi karibuni alidai kuwa serikali ya Rais Kenyatta imeanza kuyumba.