TANZIA: Kumhusu Dkt Joyce Laboso
NA MWANGI MUIRURI
SIKU nne tu baada ya saratani kumnyakua aliyekuwa mbunge wa Kibra Bw Ken Okoth (41), gavana wa Kaunti ya Bomet, Dkt Joyce Laboso alifariki Jumatatu alasiri katika Hospitali ya Nairobi kutokana na gonjwa lilo hilo, akiwa na umri wa miaka 58.
Kabla ya kifo chake, Dkt Laboso alikuwa akipokea matibabu nchini Uingereza na India tangu Mei 29 kabla ya kurejea nchini Julai 14. Mwili wake umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee, Nairobi.
Taifa Leo Dijitali imefuatilia maisha ya mwanasiasa huyu kutoka utotoni hadi alipojitosa katika bahari ya siasa.Joyce Laboso alizaliwa Novemba 25, 1960, eneobunge la Sotik na amekuwa mkewe Bw Edwin Abonyo.
Licha ya wengi kuteta mwaka 2017 alikuwa akiwania ugavana Bomet badala ya Nyanza kwa mumewe, aliishia kuungwa mkono kwa dhati na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto hadi akafanikiwa kumbwaga Bw Isaac Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2017.
Kuingia kwake ndani ya siasa kulikuwa baada ya kifo cha dadake, Lorna Laboso ambaye aliaga dunia akiwa na Kipkalya Kones katika mkasa wa ndege eneo la Narok mwaka wa 2008.
Joyce alikuwa katika Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza kati ya 2002 na 2006 kwa uzamili wa Lugha na Masuala ya Jinsia.
Kati ya 1989 na 1991 alikuwa katika Chuo Kikuu cha Reading nchini Uingereza kwa Uzamili wa Masuala ya Kiingereza kama Lugha ya Kigeni.
Kati ya 1984 na 1985 alikuwa katika Chuo Kikuu cha Paul Valery, Montpellier kwa Diploma kuhusu Lugha ya Kifaransa.
Kati ya 1980 na 1983 alikuwa akisaka digrii kuhusu Lugha na pia ualimu, hii ikiwa ni baada ya kufuzu kutoka shule ya Sekondari ya Kenya High.
Alipitia pia katika shule ya sekondari ya Kaplong Girls huku elimu ya msingi akiiasaka kutoka shule za msingi za Kaplong na Molo.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kati ya 1980 na 1983 na kusomea Shahada ya Elimu katika lugha ya Kifaransa na Fasihi.
Alikuwa ndani ya ajira ya Chuo kikuu cha Egerton katika kitengo cha ufundishaji fasihi.
Kati ya 2003 na 2006 alikuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Farrow House Education Center, Hull, Uingereza na akawa naibu mkuu wa kitengo cha wanafunzi kati ya 2001 na 2002 katika Chuo Kikuu cha Egerton.
Kuanzia 1990 alikuwa mhadhiri katika Chuo hicho cha Egerton huku kati ya 1985 na 1989 akiwa mwalimu katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kipsigis.
Atakumbukwa kama mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa Naibu wa Spika katika bunge la kitaifa akiwa mbunge wa Sotik kuanzia 2013.
Alikuwa kati ya magavana watatu wanawake wa kwanza kushinda kiti hicho. Wengine ni Anne Waiguru (Kirinyaga) na Charity Ngilu (Kitui).
Sote hapa Taifa Leo Dijitali tunatuma risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa mwanasiasa huyu aliyejitolea kuwahudumia wakazi wa Bomet.