Habari

TSC yawaonya walimu wake wanaojihusisha na vitendo vya kusaidia watahiniwa kudanganya

November 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

TUME ya Kuajiri Walimu (TSC) imewaonya walimu wakuu wa shule za sekondari na wasimamizi pamoja na waangalizi wa karatasi za mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) dhidi ya kusaidia baadhi ya watahiniwa kujihusisha na udanganyifu.

Afisa Mkuu Mtendaji Nancy Macharia amesema Jumanne asubuhi kwamba wiki jana TSC iliwachukulia hatua walimu wakuu wanne, wasimamizi watano na waangalizi kadha wa karibu wa watahiniwa waliojaribu kujihusisha katika vitendo vya udanganyifu katika mtihani.

“Tumechukua hatua kukabiliana na watu hao kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizoko. Leo Jumanne, licha ya mvua Mombasa kila kitu kinaendelea jinsi inavyofaa,” amesema Bi Macharia.

Amesema TSC inashirikiana na Wizara ya Elimu kuhusiana na matukio ya mkasa ambapo katika baadhi ya shule nchini, watahiniwa waliokuwa katika maabara Ijumaa wiki jana walipata majeraha kwa kupumua gesi ya kemikali iliyotumika katika somo la Kemia. Kemikali hiyo ni Xylene.

“Ninawahakikishia walimu kwamba tumezungumza na wizara na waziri Prof George Magoha analifuatilia suala hili kwa karibu,” amesema mkuu huyo wa TSC.

Vilevile amewapongeza baadhi ya walimu na vyombo vya usalama kwa kuchangia pakubwa kuzima visa vya udanganyifu katika baadhi ya maeneo.

“Ninawapongeza walimu na maafisa waliozuia udanganyifu kutokea katika baadhi ya shule Nairobi na Kisii,” amesema.

Macharia amesimamia shughuli ya uchukuzi wa karatasi za mtihani katika Majengo ya Uhuru na Kazi, Mombasa.