Habari

Tukosoeni kwa heshima, Mbunge Mai Mai awahimiza vijana

Na STANLEY NGOTHO April 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Kajiado Mashariki Kakuta Mai Mai amewaomba vijana humu chini kukosoa viongozi kwa njia ya heshima kupitia mitandao ya kijamii.

Akiongea mjini Kitengela wakati wa kupeana basari za thamani ya Sh33 milioni kwa wanafunzi 6,100 kama matayarisho ya mapema ya muhula ujao, mbunge huyo alisema baadhi ya vijana wanatumia mitandao kuchochea na kuchafulia viongozi majina.

Imekuwa desturi kwa baadhi ya vijana kutumia mitandao visivyo kuwachafulia viongozi majina. Hii ni hatari kubwa kwa taifa linalostawi – Mbunge wa Kajiado Mashariki Kakuta Mai Mai

Aliwaomba vijana kutumia mitandao kujinufaisha na kupasha habari za uhakika na sio kupotosha wananchi.

“Kama mzazi nawashauri vijana kujiepusha kutumiwa vibaya na kutumia mitandao kujinufaisha. Kuna mengi mazuri kwa mitandao,” aliongeza.

Vile vile, mbunge huyo aliwaomba wabunge wenzake kuhakikisha fedha za NG/CDF zimelindwa kikatiba kwani fedha hizo zimekuwa zikiimarisha maisha ya wananchi mashinani.

“Hivi sasa wanafunzi kutoka familia maskini Kajiado Mashariki watafika shuleni kwa muhula wa pili bila wasiwasi wa karo. Fedha za CDF zimeleta manufaa kwa wananchi mashinani na ni heri zilindwe kikatiba,” alisema.

Naibu Kamishina wa Isinya Michael Yator alisema matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamekuwa donda sugu miongoni mwa baadhi ya vijana suala ambalo ni hatari kwa jamii na taifa kwa jumla.

“Ni vizuri kukosoa viongozi lakini cheche za matusi mitandaoni ni hatari kwa jamii na taifa,” alisema Bw Yator.