Habari

Tunajizatiti kukomboa machifu waliotekwa ila hatuna mpango kutuma jeshi – Katibu

Na MANASE OTSIALO March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIBU wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omolo, amekanusha madai kwamba serikali imeacha juhudi za kuwaokoa machifu watano wa Mandera waliotekwa nyara na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Akizungumza katika kipindi cha asubuhi cha KTN jana, Dkt Omolo alisema serikali haijaacha operesheni ya kuwaokoa machifu waliotekwa.

“Kumekuwa na ukimya kuhusu suala la machifu waliotekwa nyara, lakini kuna shughuli nyingi zinazoendelea, ingawa hatuwezi kuzijadili moja kwa moja kwenye runinga,” alisema Dkt Omolo.

Alieleza kuwa serikali hainuii kutumia nguvu za kijeshi kuvamia maeneo yanayojulikana kuwa wanazuiliwa ndani ya Somalia ili kuwaokoa.

“Ingawa tunazingatia kuhakikisha nchi iko salama, hatutaki kupoteza maisha ambayo tungeweza kuyaokoa,” alisema.

Dkt Omolo alisema serikali bado imejitolea kuhakikisha machifu hao wanaokolewa na kwamba maafisa wa serikali nchini Somalia wanahusika katika mazungumzo.

“Tunashirikiana mara kwa mara. Watekaji walivuka mpaka kuingia nchi jirani, lakini mipaka ni alama tu za muda kati ya mataifa, kwani jamii zina mahusiano ya karibu,” alisema.

Aliongeza: “Kuna mazungumzo yanayoendelea kuhakikisha hatimaye wanarejea nchini salama na kuendelea na majukumu yao.”

Kwa mujibu wa Dkt Omolo, utekaji wa machifu hao watano ni suala linalomhusu kila mmoja, ikiwa ni pamoja na serikali, na alikiri kuwa utekaji wa maafisa wa utawala ni ishara kuwa hakuna mtu aliye salama dhidi ya tishio la Al-Shabaab.

“Usalama ni jukumu la kila mmoja wetu, na hawa ni machifu wanaofanya kazi katika wizara inayohusika na usalama. Hii inaonyesha kuwa hakuna mtu aliye salama kabisa dhidi ya vitisho hivi,” alisema.

Kwa mujibu wa katibu huyo, ugaidi ni tatizo tata, na serikali inafanya kila iwezalo kuepuka hali inayoweza kuhatarisha maisha ya maafisa waliotekwa.

Licha ya Katibu Omolo kuthibitisha kujitolea kwa serikali kuwaokoa machifu hao, familia zao huko Mandera zinasema hazijasikia chochote kutoka kwa serikali.

“Hatujaona hata afisa mmoja wa serikali akitutembelea na kutupa taarifa kuhusu juhudi za kuwatafuta wapendwa wetu,” alisema Mohamed Okash, jamaa wa mmoja wa machifu waliotekwa akizungumza kwa simu.

Kwa mujibu wa Okash, kundi la wazee waliotumwa Somalia na jamii bado hawajakutana na wawakilishi wa magaidi hao.

“Tunachojua kwa sasa ni kwamba wapendwa wetu bado wako hai lakini wanashikiliwa katika maeneo tofauti huko Jilib,” alisema.

Mnamo Februari 4, Rais William Ruto aliamuru Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Gilbert Masengeli, kuongoza operesheni ya uokoaji.

Miongoni mwa machifu waliotekwa ni Adawa Abdi Mohamed, Mohamed Hassan Kalumia, Mohamednur Hache, Abdi Hassan Suraw na Ibrahim Gabow.

Kuhusu kurejea kwa ghafla kwa MCA wa Wajir aliyekuwa ametoweka kwa takriban miezi sita, Dkt Omolo alisema idara za usalama za serikali zina hamu ya kusikia simulizi yake.

“Itakuwa vyema kujua ni nini hasa kilichotokea katika kipindi cha miezi sita. Wakati fulani, tulipata mwili wa mtu mmoja huko Wajir, na mtu anaweza kujiuliza ikiwa kulikuwa na MCA wawili, mmoja akitekwa na kuuawa, na mwingine akitekwa lakini hatimaye akarejea. Ni muhimu kuwawajibisha watu,” alisema bila kufafanua zaidi.

“Si sera ya serikali kuteka watu, na pale ambapo kuna matumizi ya nguvu kupita kiasi, tuna mifumo madhubuti ya kuwawajibisha maafisa wa serikali,” aliongeza, akikanusha madai ya kuhusika kwa serikali katika utekaji nyara.