HabariKimataifa

Tutajiapisha kama Raila Odinga, upinzani nchini Venezuela wasema

February 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA wa Upinzani nchini Venezuela wametangaza kuwa watamuiga kinara wa National Super Alliance (NASA) Raila Odinga kwa kuapisha mwaniaji wao ikiwa Rais Nicolas Maduro  ataiba kura katika uchaguzi ujao.

Mwanaharakati wa kisiasa wa Upinzani ambaye ni Meya wa zamani wa Caracas nchini Venezuela,  David Smolansky ambaye sasa anaishi uhamishoni nchini Amerika, Jumatano alisema kuwa Bw Odinga amekuwa kielelezo kwao kwa kujiapisha kuwa ‘rais wa wananchi’ baada ya kuwepo kwa udanganyifu wa kura.

Bw Smolansky aliyekuwa akizungumza katika mahojiano na kipindi cha HARDtalk katika runinga ya BBC, alisema Upinzani pia utasusia uchaguzi uliopangwa kufanyika Aprili 22, 2018.

Mwanaharakati wa kisiasa wa Upinzani nchini Venezuela, Bw David Smolansky akihutubu awali. Picha/ Hisani

“Rais Maduro aliteua na kuweka wendani wake katka tume ya uchaguzi hivyo hakuna haja ya kushiriki uchaguzi ambao tayari matokeo yake yanajulikana. Tutaiga mfano wa Kenya na kuapisha rais wetu,” akasema Bw Smolansky.

Mwanasiasa huyo alisema upinzani utaapisha rais wake na kuteua baraza la mawaziri.

“Tutakuwa na serikali mbili na sisi tutatuma ombi kwa Umoja wa Mataifa (UN) kututambua kama taifa lililojitegemea.

“Tutatafuta misaada kutoka kwa mataifa rafiki na kuendesha serikali yetu sambamba. Tumefurahishwa mno na kinachoendelea nchini Kenya,” akasema.

Rais Maduro, 55, ambaye amekuwa mamlakani tangu 2013 kutoka kwa Rais Hugo Chavez, anapigiwa upatu kushinda uchaguzi wa Aprili.

Maduro alikuwa dereva wa basi na kiongozi wa chama cha kutetea wafanyakazi kabla ya kuchaguliwa kuwa rais.

Wanasiasa wa Upinzani Henry Ramos na Henri Falcon wametangaza kuwania urais. Lakini Rais Maduro amelaumiwa kwa kuwazuia kuwania wanasiasa wa Upinzani wenye ushawishi Leopoldo Lopez na Henrique Capriles.