Ubomoaji katili
Na CHARLES WASONGA
SAA chache baada ya Mahakama Kuu kutoa amri ya kusitishwa kwa ubomoaji zaidi katika kitongoji cha Kariobangi Sewerage, mtaani Kariobangi North, ujenzi wa ua kuzunguka eneo hilo umeanza, huku nao baadhi ya watu Ruai wakionja makali ya ubomoaji.
Na Jumamosi, matingatinga ya Kampuni ya Maji na Majitaka Nairobi (NCWSC) yalikuwa yakiendelea kuangusha mabanda ya wafanyabiashara wa soko la Korogocho na kuchimba mitaro ya kujenga ua. Wanatumia saruji kuweka ukuta huo.
“Sisi tumepewa kazi na tajiri wetu tujenge ukuta kulizunguka eneo hili. Hatuna habari zozote kuhusu mivutano kuhusu umiliki wake,” akasema nyapara mmoja anayewasimamia wafanyakazi hao wa ujenzi na ambaye alidinda kujitambulisha.
Umiliki wa kipande hicho cha ardhi cha ukubwa wa ekara 10.6 unazozaniwa na jumla familia 5,000 na kampuni ya NCWSC.
Majuma mawili yaliyopita matingatinga ya kampuni hiyo yalibomoa makazi ya watu hao chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mnamo Ijumaa, Mahakama Kuu ilitoa amri ya kusitisha ubomoaji zaidi katika mtaa huo hadi kesi iliyowasilishwa na wakazi itakaposikizwa na kuamuliwa.
Mahakama hiyo ilisema kesi hiyo itasikiziwa kupitia mitandaoni mbele ya Jaji Samson Okong’o mnamo Juni 2, 2020.
Na mnamo Jumatano wiki ambayo imekamilika, Waziri wa Usalama Fred Matiang’i alikutana na Mshirikishi wa Nairobi Wilson Njenga na kutangaza kusitishwa kwa ubomoaji au shughuli zozote katika kipande hicho cha ardhi.
Hii ni baada ya wakazi waliofurushwa kufanya maandamano kulaani serikali kwa kile walichosema ni kutendewa “unyama wakati huu mgumu wa janga la Covid-19.”
Kampuni hiyo inadai ardhi hiyo ni mali yake na ilinyakuliwa na wakazi hao chini ya muungano wao kwa jina Kariobangi Sewerage Self Help Group mnamo 2008.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Waziri wa Maji Sicily Kariuki aliyesema kuwa kampuni hiyo inapania kujenga mradi kusafisha majitaka katika kipande hicho cha ardhi.
Wakati huo huo, mamia ya wakazi usiku wa kuamkia Jumamosi waliachwa bila makao katika eneo la Ruai baada ya serikali kubomoa nyumba zao.
Ubomoaji huo ulianza usiku wa kuamkia Jumamosi na kuendelea hadi majira ya asubuhi.
Wakazi hao walisema wamekuwa wakiishi katika kipande hicho cha ardhi tangu mwaka wa 2008 na wana stakabadhi halali.
Picha kutoka eneo hilo pia zinaonyesha wanawake na watoto wakihangaika bila pa kutafuta hifadhi.
Ardhi hiyo pia inasemekana kumilikiwa na kampuni ya NCWSC.
Mapema mwaka 2020 Serikali ilianza kuwafurushwa watu ambao walinunua ardhi karibu ardhi ya ukubwa wa ekari 3,000 ili kutoa nafasi kwa upanuzi wa mradi wa kusafisha majitaka katika eneo la Ruai, Nairobi.