Uchaguzi wa 2027: Biashara ya vyama yanoga 119 vikisajiliwa
IDADI ya vyama vya kisiasa inaongezeka kwa kasi huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.
Hadi sasa, kuna jumla ya vyama 119, hali inayoashiria si tu upana wa demokrasia, bali pia biashara inayozidi kushamiri katika siasa na thamani kubwa ya ushawishi wa kisiasa.
Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bw John Cox Lorionokou, anasema Kenya ina vyama 92 vilivyosajiliwa kikamilifu na vingine 27 vina usajili wa muda, jumla ikiwa vyama 119.
Rekodi zinaonyesha mabadiliko makubwa lakini ya kimyakimya katika taswira ya kisiasa nchini.
Mbali na mikutano ya hadhara, miungano na mikakati ya urais, kuna sekta inayokua kwa kasi lakini huzungumziwa kwa tahadhari: biashara ya vyama vya kisiasa.
Usajili wa vyama vipya unasukumwa si kwa misingi ya itikadi pekee, bali pia fedha, ushawishi na mikakati ya kujiokoa kisiasa.
Chanzo kikuu cha mvuto huu ni ufadhili wa umma.
Vyama vinavyokidhi vigezo vya kisheria hunufaika na Hazina ya Vyama vya Kisiasa.
Katika mwaka wa kifedha wa 2025/2026, UDA na ODM vilipata mgao mkubwa zaidi wa jumla ya Sh1.2 bilioni. UDA ilipata zaidi ya Sh789 milioni huku ODM ikipata Sh421 milioni.
Vyama vingine kama Jubilee, Wiper, DAP-K, Ford Kenya na Kanu vilipata mgao mdogo, huku vyama vidogo vikilalamikia mfumo wa kugawa pesa za hazina hiyo. Baadhi yao hata waliwasilisha ombi bungeni wakitaka marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa wakisema mfumo wa ufadhili unavipendelea vyama vikubwa.
Hata hivyo, ufadhili si kivutio pekee. Usajili wa chama unatoa mamlaka ya kisheria ya kuteua wagombeaji.
Kipindi cha uteuzi kimekuwa chanzo kikubwa cha mapato, huku wagombeaji wakilipa ada kubwa ili kupata tiketi.
Katika vyama vyenye ushindani mdogo wa ndani, uongozi hudhibiti kikamilifu uteuzi, na kuugeuza kuwa chombo cha kisiasa na kibiashara.
Wachambuzi wanasema kuongezeka kwa vyama kunachochewa pia na migogoro ya ndani ya vyama vikubwa, uteuzi usio wa haki na ukosefu wa demokrasia ya ndani.
Wanasiasa wengi huanzisha vyama vyao ili kujilinda dhidi ya kunyimwa tiketi.
Kwa wengine, chama cha kisiasa ni rasilmali ya muda mrefu, inayoweza kuuzwa, kuunganishwa au kutumika katika mazungumzo ya miungano.
Umiliki wa chama pia umegeuka kuwa alama ya hadhi, ukimpa mwanasiasa nafasi ya kutambuliwa kama mhimili wa maamuzi.
Hata hivyo, wakosoaji wanaonya kuwa kibiashara cha vyama inaweza kudhoofisha demokrasia.
Uchaguzi wa 2027 unavyokaribia, biashara ya vyama vya kisiasa inaonyesha wazi kuwa katika siasa za Kenya, chama si jukwaa pekee, bali ni mali.