Habari

Uchu wa raia kumiliki bunduki na jinsi ambavyo wanatapeliwa

June 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

MJADALA unaoendelea nchini Kenya kuhusu ufaafu au ubutu wa kuwahami askari rungu umechora taswira ya jinsi wengi hupenda bunduki.

Bunduki huaminika na wengi kuwa silaha tosha ya kujiepusha na masaibu mengi pamoja na uwezo wa kukabiliana na wahalifu.

Wapo wanayoiona kuwa ni ya kupendeza kijumla.

Ni silaha ambayo Inspekta Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai anaonya raia wafahamu “sio mwiko wa kutumika kusonga ugali.”

“Ukicheza nayo utajipata pabaya sana kiafya,” anatahadharisha Mutyambai.

Bw Mutyambai alisema hayo akitangaza kuwapokonya bunduki askari wote wa akiba ili wapigwe msasa na hatimaye wale watakaotimiza vigezo vya msasa huo warejeshewe bunduki hizo.

Mapenzi ya raia kwa bunduki hujiangazia tena katika sera kadha za serikali; ya hivi majuzi ikiwa ni ya kuwapokonya wote ambao wanamiliki bunduki lakini hawako katika vitengo vya kiusalama ili nao wapigwe msasa. Ni hatua iliyosababisha wengi – hasa wanasiasa na wafanyabiashara mashuhuri – kukimbia mahakamani kupinga hatua hiyo.

Hali hii ya Wakenya kupenda kujihami kwa bunduki imezua kero kuu ya kiusalama ambapo magenge kila kuchao yanazuka yakivamia kila mahali kuliko na uwezekano wa kuwa na bunduki, maafisa wa polisi wakijipata pabaya wakilengwa na kuuawa wakipokonywa silaha zao.

Ni katika hali hiyo ambapo Kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu, Abdi Hassan anateta kuwa raia hapa wanatapeliwa kwa kiwango kikuu wakiahidiwa bunduki iwapo watatuma pesa kwa nambari fulani.

“Kuna makundi ya matapeli ambayo yamezuka hapa Uasin Gishu na ambayo kazi yao kuu ni kujifanya eti wao ni Makamishna wa Kaunti. Wanasema wanaitwa Abdi Hassan na wana bunduki za kutoa kwa wafanyabiashara mashuhuri. Nao wafanyabiashara hao wanawaamini na kutii maelekezo ya wakora hao,” anasema Barre.

Anasema kuwa wale wanaolengwa wanatakiwa watume kati ya Sh100,000 na Sh300,000 ili wapewe bunduki za kujihami.

“Ubaya ni kwamba, kuna wale ambao wamejawa na ubutu wa kimaisha kiasi kwamba wanatuma pesa hizo. Wanaambiwa wakutane mitaani ili wapewe bunduki zao. Mtu anakupigia simu akikwambia mkutane nje ya soko au kando mwa barabara ili akupe bunduki. Waza hilo: Eti Kamishna wa Kaunti anakuambia mkutane kando mwa soko au nyuma ya maduka…” anasema.

Anasema kuwa ametoa amri kwa maafisa wote wa usalama wawajibikie suala hilo na wawasakame wote ambao wanaendeleza njama hiyo.

Pia, anaonya kuwa kumejaa matapeli wa kuombea pesa za wenyewe ziongezeke.

“Tangu lini ukasikia pesa ikizalishwa kwa kuombewa mitaani na wahubiri bandia? Ukiangalia hao wanaokuambia wataombea pesa zako wao ndio wangeanza kuombea zao. Lakini unapata watu wakifuata maagizo hayo ya matapeli na kuwapa pesa zao ambapo wanaishia kutapeliwa,” akateta.

Mshukiwa asakwa

Hali ni hiyo katika Kaunti za Bomet na Murang’a ambapo vitengo vya usalama vinamsaka mshukiwa wa kiume ambaye amekuwa akitapeli wafanyabiashara maarufu wa eneo hilo akiwaahidi kuwapa bunduki za kujilinda.

Imeripotiwa kwamba mshukiwa huyo amekuwa akiwapigia simu wafanyabiashara hao akijifanya kuwa kamanda wa polisi wa Murang’a, na Bomet ambao ni Josephat Kinyua na Naomi Ichami mtawalia na ambao wako na mpango huo wa kuwahami wafanyabiashara.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Mohammed Barre, mwanamume huyo ambaye kwa sasa hawajafanikiwa kumnasa ametapeli wafanyabiashara kadha katika njama hiyo ya hadaa.

Alisema kuwa mwanamume huyo akimlenga mwathiriwa wa utapeli huo, humwagiza atume Sh4,000 za kuidhinisha cheti cha kinidhamu na Sh10, 500 za mafunzo ya utumiaji bunduki na pia gharama za kuratibu uidhinishaji.

“Ni njama ya kutapeli Sh14, 500 kutoka kwa mwaathiriwa mmoja na tayari tumepata malalamishi ya wafanyabiashara 18. Kuna wengine ambao tunashuku pesa zao zilizama katika utapeli huo wa mwezi mmoja sasa na wakaamua kunyamaza,” akasema Barre.

Kamishna huyo alisema kuwa njama hiyo ilianza kutibuka wakati baadhi ya walengwa waligundua kuwa Ichami sio mwanamume bali ni mwanamke na hivyo basi shaka zao zikawasilishwa kwa maafisa wa kiusalama kumhusu mtekelezaji huyo wa njama hiyo.

“Ndio sababu tumezindua uchunguzi wa kina kuhusu mkora huyo na kwa hakika tutamnasa. Aidha awe ndani ya kikosi cha kiusalama chochote, awe raia au awe nani. Tutamnasa tu,” akasema.

Alisema kuwa juhudi za kuhami raia kwa bunduki hazitekelezwi kupitia kwa mawakala bali ni suala la uwazi na ambalo huanza na anayetaka huduma hiyo kutuma ombi kupitia kwa Kamishna wa Wilaya.

“Ombi hilo hupigwa msasa na jopo maalum la kamati ya kiusalama ya Kaunti ndogo na hatimaye ukaguzi wa utimizaji wa matakwa ya kupewa bunduki unatekelezwa na hatimaye ukifaulu, unapewa bunduki,” akasema.

Aliwataka wenyeji wakae chonjo na wakifanikiwa kumnasa mshukiwa huyo anayesakwa, wamuwasilishe kwa maafisa wa polisi.

“Ushirikiano mwema ambao maafisa wetu wanapata kutoka kwa raia umetuwezesha kutegua kitendawili vingi vya kiusalama katika Kaunti hii. Hata kwa hili, najua tutapata dokezi muhimu na tufanikiwe kumnasa mkora huyu wa uigizaji kinyume cha sheria akitumia majina ya maafisa wakuu vitengoni vya kiusalama,” akasema.