UFISADI: Magavana wataka 'waheshimiwe' wanapokamatwa
Na JUSTUS OCHIENG
MAGAVANA wanataka “wapewe heshima” wakati wanapokamatwa kwa madai ya kuhusika kwenye kashfa za ufisadi.
Kufuatia kisa cha wiki iliyopita ambapo Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu alikamatwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), magavana sasa wanataka endapo kutakuwa na mwenzao mwingine atakayekamatwa afanyiwe hivyo kwa heshima.
Kupitia kwa Baraza la Magavana, viongozi hao wa kaunti walisema hawaungi mkono ufisadi lakini pia si haki kwao kuchukuliwa kama wahalifu wenye hatia hata kabla kufikishwa mahakamani.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Wycliffe Oparanya alisema wamejitolea kupambana na ufisadi lakini akasisitiza inahitajika waheshimiwe kwa kuzingatia mamlaka ya uongozi wanayoshikilia.
“Sisi hatutetei ufisadi na tuko tayari kupigana vita dhidi yake, lakini jinsi Waititu alivyokamatwa, akatembezwa hadharani, ilikuwa ni kumkosea utu hasa ikizingatiwa mamlaka yake,” akasema Bw Oparanya kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Aliongeza: “Mbona wasifanye kazi zao kwa uungwana? Mwiteni tu gavana, mwambieni mnataka kwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi badala ya kutuonyesha vioja hivi vyote mbele ya vyombo vya habari.”
Alilalamika kuhusu majasusi wa EACC kuhusu jinsi wanavyopenda kuita wanahabari kuangazia wanavyokamata washukiwa na kupeperusha matukio hayo moja kwa moja kwenye runinga.
“Mbona wana lazima kufanya kazi yao mbele ya vyombo vya habari? Hiyo ni kusudi kuaibisha viongozi wa kaunti,” akasema.
Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Twalib Mbarak alidai Bw Waititu alipeana kandarasi zilizogharimu mlipaushuru Sh588 milioni kinyume na sheria kwa makampuni yanayohusiana naye na jamaa zake wa karibu.
Magavana wengine wanaopelelezwa kuhusu matumizi ya fedha za umma ni Mwangi Wa Iria (Murang’a), Charity Ngilu (Kitui), Muthomi Njuki (Tharaka-Nithi) na Okoth Obado (Migori).
Mwaka uliopita, magavana walilalamika kuhusu jinsi walivyokuwa wakikaamtwa kuhusiana na ufisadi wakapendekeza kesi zao zisitishwe hadi wakati watakapoondoka mamlakani.
Bw Oparanya ambaye pia ni Gavana wa Kaunti ya Kakamega, jana alisisitiza haifai magavana kuchukuliwa kama wahalifu mikononi mwa wapelelezi wakati ambapo hawajahukumiwa.
“Mnamtembeza gavana mbele ya wapigakura wake na familia? Hiyo si haki. Mnamfanya aonekane kama kwamba ana hatia wakati hata hajashtakiwa. Kwa maoni yangu tabia hiyo ni mbaya na inafaa tuonyeshwe taadhima,” akasema.
Kwenye uchunguzi kumhusu Bw Waititu, ilibainika kwamba wapelelezi wanataka kuchunguza akaunti zake za benki na zile za jamaa zake na wandani wake.
Mabenki kadhaa tayari yametakiwa kuwasilisha ripoti kuhusu shughuli zote za kifedha zilizofanyika kwenye akaunti zinazolengwa.
EACC inachunguza pia mali za gavana huyo ikiwemo majumba ya kifahari ambayo inadaiwa anajenga katika mtaa wa Runda, Hoteli ya Delta iliyo katikati ya jiji la Nairobi na hoteli nyingine ya kifahari iliyo Naivasha ili kubainisha kama zinamilikiwa kihalali.