HabariSiasa

UFISADI: Raila amtia Uhuru presha awatimue 'marafiki' zake

February 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MUUNGANO wa NASA, unaoongozwa na Raila Odinga, umemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwafuta kazi bila kusita mawaziri wote na maafisa serikalini, ambao wamehusishwa na uporaji wa mabilioni ya pesa za umma.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari jana, NASA ilitaja Baraza la Mawaziri kama “genge la majambazi” huku Bw Odinga naye akiwataja waporaji wa mali ya umma kama “wahalifu wasiostahili huruma.”

“Sasa ni wazi kuwa shughuli kuu ya mawaziri ni uporaji. Kwa hivyo, ni sawa kusema kuwa Baraza la Mawaziri limegeuka kuwa genge la majambazi, ambao bila huruma wanapora pesa za umma,” ikasema taarifa iliyotumwa na afisa mkuu wa NASA, Norman Magaya.

Msimamo huu mkali ni kinyume na jinsi Bw Odinga amekuwa akikosoa Serikali ya Jubilee tangu aliposalimiana na Rais Kenyatta mwaka jana.

“Tunamhimiza Rais achukue hatua sasa, na kuiga nchi ambazo zimefanikiwa kushinda vita dhidi ya ufisadi. Mawaziri wote na maafisa wa ngazi za juu serikalini, ambao wamehusishwa na ufisadi ni lazima wafutwe kazi mara moja, kisha wafanyiwe uchunguzi wa kina,” ilisema taarifa hiyo iliyotumwa na afisa mkuu, Norman Magaya.

Kulingana na NASA, viwango vya ufisadi nchini vinatisha, na vimezima ndoto na matarajio ya Wakenya kuhusu hali ya baadaye ya taifa lao.

Akiongea kwenye hafla tofauti jana, Bw Odinga alionya kuwa kwamba msingi wa Kenya kama taifa umo hatarini, ikiwa watu wanaoshukiwa kushiriki ufisadi hawatakabiliwa kisheria na kutupwa gerezani.

Akihutubu kweye Kongamano la Vyama vya Wafanyakazi Afrika kuhusu Elimu (PANAF) jijini Nairobi, Bw Odinga aliwataja watu hao kuwa wahalifu wanaopaswa kukabiliwa bila huruma.

“Tumechoshwa na ripoti kuhusu ufisadi kila mara. Waporaji wa mali ya umma ni sawa na wahalifu wanaotishia kusambaratisha msingi wa nchi yetu. Ni lazima tubadilishe mkakati wa vita hivyo,” akasema.

Alieleza kwamba ni lazima Kenya ishirikiane na nchi ambazo washukiwa hao wanadaiwa kuficha fedha wanazopora, ili kufanikiwa kukomesha wizi wa mali ya umma.

Bw Odinga alisema ufisadi si tatizo la Kenya pekee barani Afrika, hivyo lazima iimarishe mbinu za kuukabili.

“Kuna nchi nyingi zinazoathirika na ufisadi barani, lakini zimefanikiwa kuukabili. Mfano bora ni Afrika Kusini, ambapo hata aliyekuwa rais Jacob Zuma anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi,” akasema Bw Odinga.

Naye kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi aliongeza shinikizo hizo kwa Rais Kenyatta akimwambia aonyeshe kwa vitendo kuwa ana nia na uwezo wa kukomesha ufisadi.

“Ni lazima Rais aonyeshe kuwa sio Wakenya anaochezea sarakasi kwa maneno matupu, wakati taifa linapokabiliwa na janga,” akasema Bw Mudavadi kwenye taarifa.

Alimtaka Rais Kenyatta kuwafuta mawaziri na wengine ndani ya serikali yake waliohusishwa na uporaji.

“Ni lazima Rais awafute kazi mara moja. Ni kinaya kuwachunguza watu wakiwa wangali ofisini. Watatumia kila mbinu kuvuruga uchunguzi,” alisema Bw Mudavadi.

Wakenya wa kawaida nao hawakuachwa nyuma kwani walianzisha kampeni kwenye mitandao kumtia presha Rais achukue hatua kali dhidi ya wezi wa mali ya umma ndani ya serikali yake.

Kwenye mtandao wa Twitter, Wakenya walieleza hisia zao kupitia mjadala #PleaseSackTheseCSs.

“Rais Kenyatta, juhudi zako za kupambana na rushwa zinazuiwa na mawaziri wako mwenyewe. Tumengoja uchukue hatua dhidi yao lakini tumechoka. Tafadhali wafute kazi,” akasema David Osiany.

Kwenye mtandao wa Facebook, wengi walitoa hisia kama hizo, wakisema kwamba imefikia wakati Rais kuwafuta kazi mawaziri hao, bila kujali uhusiano alio nao.

Mnamo 2015 wakati baadhi ya mawaziri waliposhukiwa kushiriki ufisadi, Rais Kenyatta aliwaambia wajiondoe kwenye Baraza la Mawaziri ili kufanikisha uchunguzi.

Lakini safari hii Mamlaka ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) pamoja na Idara ya Upelelezi (DCI) zinawachunguza mawaziri wanaoshukiwa wakiwa bado ofisini.

DCI inaendelea kuchunguza kashfa ya uchimbaji mabwawa ya Kimwarer na Aror, katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, ambapo Kenya inakisiwa kupoteza Sh21 bilioni.