Uhalifu umepungua kwa asilimia 50 – Kibicho
Na WANDERI KAMAU
VISA vya uhalifu nchini vimepungua kwa asilimia 50 tangu serikali kuanza kutekeleza kafyu Machi, amesema Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho.
Hili ni kinyume na madai ya baadhi ya wananchi, kwamba sehemu kadhaa nchini zimekuwa zikikumbwa na ukosefu wa usalama hasa nyakati za usiku.
Wengine pia wamekuwa wakiwalaumu polisi kwa kushiriki moja kwa moja kwenye uhalifu au kushirikiana na wahalifu kutekeleza maovu hayo.
Lakini kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Jumatatu asubuhi, Dkt Kibicho amesema kuwa kinyume na hayo, takwimu walizo nazo zinaonyesha kuwa visa hivyo vimepungua maradufu, hasa kutokana na utekelezaji wa kafyu.
“Takwimu tulizo nazo kuhusu hali ya uhalifu nchini zinaonyesha kuwa umepungua kwa asilimia hamsini kati ya Machi na Aprili 2020. Hivyo, polisi hawapaswi kuelekezewa lawama kutokana na utovu wa nidhamu wa polisi mmoja,” amesema.
Ameeleza kuwa ni vigumu kwa wahalifu kuendesha maovu yao nyakati za usiku, ikizingatiwa kuwa baadhi ya maagizo ambayo maafisa wa usalama wamepewa ni kulinda mali ya wananchi.
Wiki iliyopita, baadhi ya wakazi Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, walilalamikia ongezeko la visa vya uhalifu, wakisema kuwa wahalifu wamekuwa wakivunja maduka yao licha ya uwepo wa maafisa wa usalama wanaopiga doria.
Visa vya unywaji pombe haramu pia vimeripotiwa kuchipuka upya katika baadhi ya sehemu za Kati na mitaa duni ya jiji la Nairobi.
Wakati huo huo, serikali imeonya kuwa huenda ikaongeza muda wa kutekeleza kafyu na marufuku ya kutotoka ama kuingia katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi, Kwale na Mandera, ikiwa visa vya maambukizi havitapungua.
Mnamo Jumamosi, Rais Uhuru Kenyatta aliongeza utekelezaji wa maagizo hayo kwa siku 21 zaidi, hadi wakati maambukizi hayo yatapungua.
Na sasa, Dkt Kibicho amesema kuwa hata baada ya muda huo kukamilika, serikali haitasita kuuongeza, ikiwa wananchi wataendelea kukaidi maagizo na kanuni ambazo zimewekwa ili kudhibiti maambukizi hayo.
“Wananchi wanapaswa kufahamu kuwa lengo kuu la serikali ni kuyalinda maisha yao wala si kuwaadhibu. Si furaha yetu kutekeleza maagizo kama kufungwa kwa baadhi ya biashara, kwani tunafahamu kuwa ni tegemeo kwa maelfu ya Wakenya. Hata hivyo, hatuna lingine kwani lazima tufanye kila tuwezalo kuhakikisha kuwa tumelinda maisha yao kupitia maamuzi hayo magumu,” akasema.
Amesema kuwa mnamo Jumapili, maafisa wa usalama waliwakamata watu 402 kwa kukiuka kanuni hizo.
Jumatatu iliyopita, watu 50 walitoroka kutoka Chuo cha Mafunzo ya Matibabu Kenya (KMTC) Nairobi, walikokuwa wamewekwa ili kudhibiti maambukizi ya corona.