Uhuru aapa kuzima Tangatanga
NDUNGU GACHANE na LEONARD ONYANGO
RAIS Uhuru Kenyatta ameapa kuanza kampeni ya kuzima wanasiasa wa kundi la Tangatanga wanaohujumu uongozi wake.
Rais Kenyatta aliyeonekana mwenye ghadhabu Jumapili alisema kuwa baadhi ya wanasiasa, hasa wa chama cha Jubilee, wamekaidi wito wake wa kutaka wasitishe kampeni za mapema na badala yake watumikie Wakenya.
Rais Kenyatta aliyekuwa akizungumza kwa lugha ya Kikuyu alisema viongozi hao ‘wakora’ wamekataa kuunga mkono juhudi zake za kutaka kuunganisha nchi kupitia handisheki.
“No riu ningwaria na Gikuyu, aya nimeke uria mekaga maturaga manumaga ni uhoro wao gutiri kundu maratutwara (Leo ninazungumza kwa lugha ya Kikuyu, acha viongozi hao wafanye wanachofanya lakini sitishiki…” akasema Rais Kenyatta.
Kiongozi wa nchi alisema kuwa hana haja ya kukatalia mamlakani lakini lengo lake kuu ni kumaliza siasa za ukabila ambazo alisema zimegawanya nchi kwa muda mrefu.
“Sina mpango wa kukatalia mamlakani au kuiba fedha za umma lakini nitahakikisha kuwa ninaacha nchi iliyoungana na kila Mkenya anaweza kwenda popote bila uwoga,” akasema Rais Kenyatta.
Rais Kenyatta aliyekuwa akizungumza uwanjani Kasarani alipokutana na waumini wa dhehebu la Akorino alisema baadhi ya wanasiasa wamemchukulia kuwa mwoga kutokana na ukimya wake.
Alisema atazunguka kote nchini kuwamaliza kisiasa wanaopinga handisheki kwa kuhimiza Wakenya wasiwachague katika uchaguzi ujao.
Kwa mara nyingine, Rais Kenyattta aliwataka viongozi hao ambao wameanza siasa za 2022 kukoma kutangatanga na kuwatumikia wananchi.
Rais Kenyatta alionekana kuwalenga wanasiasa ambao wanaunga mkono Naibu wa Rais William Ruto kuwania urais 2022.
“Leo ninazungumza kwa lugha ya nyumbani, nitaenda katika eneo langu (la Mlima Kenya) kuwaambia watu kile ambacho wanafanya.
‘Hawakunichagua’
“Wanafaa kujua kwamba si wao walionifanya kuwa rais, bali wajue kwamba mimi ndiye niliyewafanya kupata viti. Wakenya ndio walionichagua na nitaendelea kusimama na ukweli hadi nikamilishe kazi mliyonipa,” akasema Rais Kenyatta.
Alisema kuwa ataendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa kuna amani nchini Kenya na kuwezesha Wakenya kupata huduma bora za matibabu.
“Wanafikiri kwamba nikiwa kimya, wamefaulu kuninyamazisha, nimesema kwamba sitaki siasa na hiyo ndiyo maana sijawatimua katika maeneo waendayo,” akasema.
Wakati huo huo, viongozi wa kundi la Kieleweke wakiongozwa na mbunge Maalumu Maina Kamanda na mwenzake wa Cherangany Joshua Kutuny walisema kuwa wanasiasa ambao wametangaza msimamo wao wa kuunga Dkt Ruto wajiandae kupoteza viti katika uchaguzi wa 2022.
Viongozi hao, waliokuwa wameandamana na wabunge Anthony Oluoch (Mathare) na Caleb Amisi (Sabaot), walisema handisheki baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga imeleta utulivu nchini na Wakenya hawataruhusu viongozi wasiopenda amani kupata nyadhifa mwaka wa 2022.
Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika Kanisa la Kianglikana la St Thomas mtaani Huruma, Nairobi.