Habari

Uhuru afinya Raila

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga amejipata katika njia-panda kuhusiana na mvutano kuhusu mfumo mpya wa ugawaji wa fedha za kaunti.

Kwa upande mmoja, Bw Odinga anashinikizwa na mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta kuunga mkono mfumo huo mpya utakaofaa maeneo yenye watu wengi, lakini upande wa pili maseneta kutoka ngome zake za kisiasa Pwani, Nyanza na Kaskazini mwa Kenya wameapa kuupinga mfumo huo kwani utasababisha kaunti 18 za maeneo hayo kupoteza fedha.

Hali hii tete imemlazimu Bw Odinga kukatiza mapumziko yake ya kupata nafuu eneo la Watuma, Kaunti ya Kilifi na kurejea Nairobi ili kuongoza mazungumzo ya kutatua suala hilo, ambalo sasa linatisha kusambaratisha muafaka wake na Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Mpango wa Maridhiano (BBI).

Duru zilieleza Taifa Leo kwamba Bw Odinga leo Jumatatu anapanga kufanya msururu wa mikutano na maseneta wa ODM ili kupata njia mwafaka ya kutatua mvutano huo ambao pia unatishia kukwamisha shughuli katika kaunti.

“Raila pia atafanya mazungumzo na wandani wa Uhuru ili kupata muafaka kuhusu suala hilo ili aisje akalaumiwa kwamba ndiye anajuhumu handisheki na mchakato wa BBI, ambayo inahimiza usawa katika ugavi wa rasilimali,” akasema mwandani wa Bw Odinga ambaye aliomba tulibane jina lake.

Mwanasiasa huyo alikiri kuwa kiongozi huyo wa ODM anakabiliwa na hali ngumu kupata njia ya kuwashawishi maseneta kutoka kaunti 18 zitakazopoteza pesa kuunga mkono mfumo mpya anaotaka Rais Kenyatta, ili kunusuru handisheki na BBI.

“Kiongozi wetu pia ana kibarua cha kuzuia uwezekano wa wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga kuchochea kufeli kwa hoja hiyo ili kuonyesha kuwa ushirikano wake na Rais hauongozwi na maslahi ya Wakenya,” akaongeza.

Hii ni baada ya Kiranja wa Wengi katika Seneti, Irungu Kang’ata kumwonya Bw Odinga na ODM kwamba kupitishwa kwa mfumo huo kwenye kikao cha kesho ndio njia ya pekee ya kushawishi ngome za Jubilee kuendelea kuunga mkono BBI na handisheki.

“Mnamo Jumanne tutapiga moyo konde na kuwasilisha hoja kuhusu mfumo huo. Tukipoteza, bila shaka BBI itaporomoka. Tunaunga mkono BBI kwa sababu kwa mtazamo wetu inaendeleza dhana ya usawa kwa misngi ya mtu moja, shilingi moja,” akasema Bw Kang’ata mnamo Jumamosi akiwa Murang’a.

Kwa upande mwingine, Rais Kenyatta ataongoza mkutano wa kundi la maseneta wa Jubilee kesho asubuhi kabla suala hilo kuamuliwa katika kikao cha Seneti baadaye alasiri.

Lakini mwenyekiti wa ODM John Mbadi amepuuzilia mbali kauli ya Bw Kang’ata akiitaja kama vitisho visivyosaidia chochote.

“Tumewaacha maseneta wetu kuchunguza vigezo vilivyoko na kujadiliana na wenzao ili kwa pamoja wakubaliane kuhusu mfumo bora wa ugawaji fedha. Mvutano huu hauhusiani na handisheki wala BBI,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

ODM imekuwa ikitegemea handisheki katika kupitishwa kwa ripoti ya BBI ili kufanikisha ndoto ya Bw Odinga kuingia Ikulu baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022.

“Sio siri kwamba tunalenga kutumia ushirikiano wetu na Jubilee kupitia handisheki kufanikisha mageuzi yaliyopendekezwa katika ripoti ya BBI ili yamwezeshe kinara wetu Raila kuwa rais wa Kenya 2022. Lengo la chama chochote cha kisiasa huwa ni kutwaa mamlaka,” Seneta wa Siaya James Orengo alisema awali.

Wadadisi sasa wanasema sasa Bw Odinga atalazimika kutumia weledi wake wa siasa kushawishi maseneta wa kaunti za ngome zake za Pwani, Nyanza na Kaskazini kuunga mkono mfumo unaopendekezwa wa ugavi wa fedha ili kudumisha handisheki na BBI.

“Akishindwa kushawishi maseneta wa Mombasa, Kilifi, Kwale, Taita Taveta, Tana River, Mandera, Narok, Kisii, Nyamira na wengineo wanaopinga mfumo huu, atapoteza imani ya Rais Kenyatta na wandani wake. Sharti abuni mbinu za kufidia kaunti hizo zitakazopoteza sehemu ya mgao wa fedha,” akasema Bw Martin Andati.