Uhuru akoroga ngome yake kuhusu urithi
KENNEDY KIMANTHI na JAMES MURIMI
UKOSEFU wa uwazi kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhusu urithi wake ifikapo 2022, umeacha ngome yake ya Mlima Kenya kuchanganyikiwa na viongozi wengi kuamua kusajili vyama vyao vya kisiasa.
Rais Kenyatta husisitiza anajiepusha na siasa za urithi wake atakapostaafu 2022, licha ya kuwekewa presha na baadhi ya viongozi wanaomtaka atangaze wazi kama atamuunga mkono naibu wake William Ruto au la.
Imefichuka kuwa, viongozi wanaohofia kuachwa kwenye baridi serikali ijayo itakapoundwa, wameamua kujitafutia vyama vyao ambavyo wanatarajia kutumia kupata pa kujisitiri katika serikali mpya.
Wachanganuzi wa kisiasa wanasema hali hii huenda ikafanya Mlima Kenya isipige kura kwa kauli moja jinsi imekuwa kwa miaka mingi.
Kando na uundaji wa vyama vipya, vyama vingine ambavyo vililegea vilipoamua kuunga mkono Jubilee vimeanza kuimarishwa eneo hilo.
Wiki iliyopita pekee, vyama viwili vilizinduliwa na kuingia katika orodha ndefu ya vingine ambavyo vimeundwa tangu mwaka 2019.
Vile vilivyoundwa wiki iliyopita ni The Service Party of Kenya (TSP) na National Ordinary People’s Empowerment Union (Nopeu).
Wadadisi wanasema hali hii imechangiwa pia na migogoro iliyoibuka katika Chama cha Jubilee ambapo sasa kuna kambi mbili, zinazoegemea upande wa Rais Kenyatta na ule wa Dkt Ruto.
Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri alidai chama chake cha TSP hakikufadhiliwa na Dkt Ruto kama inavyodhaniwa na baadhi ya wananchi.
“Hizo ni porojo za vijijini ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu. Dkt Ruto ni rafiki yangu lakini nitawapa wakazi wa Mlima Kenya kipaumbele. Tutajadiliana kama jamii, sitaki jamii yangu inichukulie kuwa mbinafsi,” akasema.
Nopeu ambacho kinahusishwa na Mbunge wa Afrika Mashariki (EALA), Bw Mpuru Aburi, kinatarajiwa kuzindua makao makuu katika mtaa wa Lavington wiki hii.
Bw Aburi aliepuka kuthibitisha kama chama hicho ni chake.
“Ninachofahamu ni kwamba ni chama cha jamii ya Wameru ambao wamechoshwa na uongozi wa udhalimu,” akasema.
Chama cha PNU kilichotumiwa na Mwai Kibaki, kilianza kujifufua hivi majuzi baada ya kufanya uchaguzi wa viongozi wapya mwaka 2019.
Chama kingine kilichoibuka ni Civic Renewal Party (CRP) ambacho kinahusishwa na Gavana wa Murang’a Mwangi Wa Iria.
Mbunge wa Gatanga, Bw Nduati Ngugi alipuuzilia mbali vyama vinavyoibuka katika eneo la Mlima Kenya akisema eneo zima litasubiri mwelekeo wa kisiasa kutoka kwa Rais.
“Inafaa tujifunze kutoka kwa wenzetu wa Nyanza kuhusu umuhimu wa kushikilia chama kimoja. Tukimpuuza Rais katika suala hili tutajuta katika eneo hli. Tunataka Mlima Kenya izungumze kwa kauli moja kisiasa,” akasema.
Mchanganuzi wa kisiasa, Bw George Muriithi alisema endapo Mlima Kenya itagawanyika, viongozi watalazimika kufanya siasa za maendeleo kwani hawatakuwa tena na nafasi ya kutumia ukabila kujitafutia umaarufu.
“Wanasiasa watalazimika kutushawishi kimaarifa wala si kikabila wanapotafuta kura. Huo ndio utamu wa demokrasia,” akasema.