Uhuru ampa Matiang'i mamlaka ya kusimamia mawaziri na miradi yote
Na BENSON MATHEKA
Rais Uhuru Kenyatta Jumanne alimuongezea Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, mamlaka makuu kwa kumteua kusimamia kamati ya maendeleo, utekelezaji na mawasiliano katika Baraza la Mawaziri ambapo wenzake wote watakuwa chini yake.
Hatua hii inampa Bw Matiang’i uwezo wa kumulika utendakazi wa wizara zote za serikali na hivyo kumfanya kinara wa wenzake, na pia macho ya rais katika utekelezaji wake wa Ajenda Nne Kuu za Maendeleo, msimamizi wa usalama wa kitaifa pamoja na utawala wa serikali kuu mikoani na kaunti.
Kwenye agizo kuu la kwanza la rais mwaka huu, Dkt Matiang’i atakuwa akiripoti kwa Rais Kenyatta moja kwa moja kuhusu utendakazi wa kila waziri serikalini.
Kamati hiyo itakayojulikana kama Kamati ya Taifa ya Utekelezaji wa Maendeleo na Mawasiliano ya Baraza la Mawaziri, pia itashirikisha Mwanasheria Mkuu na Katibu wa Baraza la Mawaziri. Itakuwa na ofisi na wafanyakazi ambao watakuwa chini ya Bw Matiang’i.
Mamlaka haya mapya yanamfanya Bw Matiang’i kufuatilia kwa makini na kikamilifu yanayotendeka katika wizara nyingine za serikali kama alivyofanya mwaka jana alipoidhinisha sheria za usalama barabarani na kusimamia mitihani ya kitaifa.
“Ni muhimu kutoa agizo kuu la rais kueleza mfumo wa kusimamia kikamilifu, kushirikisha na kutekeleza miradi ya maendeleo ya serikali,” alisema Rais Kenyatta.
Kulingana na agizo hilo, ambalo rais alitoa akiwa Ikulu ya Mombasa, kazi ya kamati itakuwa ni kusimamia miradi yote ya maendeleo ya serikali, kupokea na kujadili ripoti za kamati tekelezi ya kiufundi ya taifa kuhusu maendeleo na kutoa mwongozo kuhusu vizingiti vinavyolemaza maendeleo ya serikali ya kitaifa.
Aidha, jukumu la kamati hiyo litakuwa ni kuhakikisha kwamba pesa zinazotengewa miradi ya maendeleo zitakuwa zikitumiwa ipasavyo na kwamba mawasiliano ya serikali yatakuwa yakifikia umma na washikadau ipasavyo.
“Kamati hii itakuwa ikifuatilia na kutathmini jinsi pesa zilizotengewa miradi ya serikali kuu zimetumiwa kwa miradi inayopaswa kupatiwa kipaumbele na kuhakikisha imetekelezwa ipasavyo,” Rais Kenyatta alisema.
Naibu wa Bw Bw Matiang’i katika kamati hiyo atakuwa ni Waziri wa Fedha Henry Rotich.
Uteuzi huo ulijiri saa chache baada ya Rais Kenyatta kuwapatia wakuu wa kanda, ambao wako chini ya Bw Matiang’i nguvu za kushirikisha maendeleo na usalama katika maeneo yao. Hatua hii itakahakikisha kuwa Bw Matiangi atashirikisha shughuli zote za serikali mashinani na kitaifa.
Rais Kenyatta pia alihamisha Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama wa Taifa (NTSA) kutoka kwa Wizara ya Uchukuzi hadi Wizara ya Usalama wa Ndani inayosimamiwa na Bw Matiang’i. Hii inamaanisha shughuli za usalama barabarani sasa ziko chini ya waziri huyo anayetambulika kama mchapa kazi hodari katika kila idara anayosimamia.
Wizara yake pia inasimamia usalama wa taifa na idara ya polisi, ujasusi na usalama. Makamanda wote wa polisi wako chini yake na ni mwanachama wa baraza la usalama la taifa. Pia makamishna wote wa kanda wamo chini yake.
Wakenya walimpongeza Rais kwa hatua hiyo wakisema Bw Matiang’i ni mchapa kazi na atamaliza ufisadi ambao umekuwa kikwazo cha maendeleo.
Rais pia aliwapa makamishna wa kaunti nguvu zaidi za kushirikisha ajenda za serikali kuu katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na usalama na mazingira.
Washirikishi hao wa mikoa na makamishna wa kaunti sasa watakuwa ndio wakuu wa vitengo kadhaa vya shughuli za serikali na pia masikio na macho ya serikali kuu mashinani.