Habari

Uhuru ana mwaka hajaenda 'nyumbani'

November 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta anakabiliwa na uasi mkubwa katika eneo la Mlima Kenya huku wakazi wakidai amewasahau licha ya kumpigia kura kwa wingi mnamo 2017.

Wakazi wanamlaumu Rais kwa kuwasahau na “kuelekeza maendeleo katika sehemu zingine nchi hasa ngome za upinzani.”

Tangu Novemba mwaka uliopita, Rais Kenyatta amefanya ziara saba pekee katika eneo hilo, huku nyingi zao zikiwa za kuhudhuria mazishi ama hafla zingine za kijamii.

Hii ni tofauti na ziara saba ambazo amefanya katika Kaunti ya Kisumu, ambako amekuwa akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Rais pia amekuwa akifanya ziara nyingi katika eneo la Pwani, ambako pia amekuwa akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo, zikiwemo barabara na miundomsingi mingine muhimu.

Mara ya mwisho kulitembelea eneo hilo ilikuwa Agosti 24, mwaka huu, alipohudhuria mazishi ya mwanamuziki maarufu John De Mathew katika eneo la Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Mnamo Desemba 2018, alihudhuria hafla ya kufuzu kwa Bw Michael Kamotho, maarufu kama “Githeriman” kutoka kituo cha kumsaidia kuacha ulevi katika Kaunti ya Kiambu.

Mnamo Februari 28 mwaka huu, aliitembelea Kaunti ya Murang’a, ambapo alihudhuria mazishi ya mfanyabiashara Kamau Thayu.

Mnamo Machi 5, Rais aliitembelea Kaunti ya Kirinyaga, kufungua Kongamamo la Ugatuzi mjini Kerugoya.

Alirejea katika kaunti iyo hiyo baadaye alipohudhuria harusi ya Gavana Anne Waiguru na wakili Kamotho Waiganjo katika eneobunge la Gichugu.

Mnamo Julai 25, alizindua tawi la Kampuni ya Kutengeneza Mafuta ya Bidco eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, alipokuwa akielekea kuhudhuria mazishi ya mamake mwanasiasa Peter Kenneth, Bi Rahab Wambui katika Kaunti ya Murang’a.

Na ingawa aliahidi kwamba angerejea katika eneo hilo Septemba kuzindua kiwanda cha kutengeza simu za rununu katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Kaunti ya Nyeri, hakutimiza hilo.

Badala yake, alirejea Agosti 24, kwa mazishi ya Bw De Mathew.

Hali ngumu kwelikweli

Kutokana na hilo, wenyeji wanalalamikia hali ngumu ya kiuchumi, hasa kutokana na kuzorota kwa sekta ya kilimo.

Wakulima wengi wanaotegemea mazao ya majani chai, kahawa, pareto, miraa na mpunga wanalalama kudorora kwa kilimo, baadhi wakisema kuwa huu ndio wakati mgumu zaidi wamewahi kupitia.

Kwa mfano, wakulima wa majani chai wanalalamikia kiwango cha chini cha bonasi walichopokea majuzi, wakilalama kwamba hali hiyo imekuwa ikidorora tangu 2017.

Kaunti zilizoathiriwa zaidi ni Nyeri na Murang’a, ambako mazao hayo hukuzwa kwa wingi.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, wakulima wanalalama kuhusu kudorora kwa zao la mpunga, baada ya kusimamishwa kwa ujenzi wa Bwawa la Thiba, ambalo Rais Kenyatta alizindua akiahidi kuwa lingeimarisha ukulima wa zao hilo.

Rais Kenyatta amekuwa ziarani katika mataifa ya kigeni, katika siku za hivi majuzi, hali ambayo baadhi ya wakazi wanadai imemfanya akose muda wa kushughulikia matakwa yao.