Uhuru ashangaza kuwaacha walinzi wake mataani
JUSTUS OCHIENG na RUSHDIE OUDIA
RAIS Uhuru Kenyatta alishangaza walinzi wake usiku wa kuamkia Jumapili wakati alipowaacha katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kisumu, na badala ya kuabiri ndege iliyokuwa ikimsubiri wakaondoka na kiongozi wa ODM Raila Odinga hadi mjini Kisumu, ambako walikaa kwa takriban saa tatu.
Rais Kenyatta alikuwa amehudhuria mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Hazina ya Maendeleo ya Vijana Bruce Odhiambo pamoja na Bw Raila na viongozi wengine wakuu katika eneo la Koru, Muhoroni katika Kaunti ya Kisumu.
Alipotoka Muhoroni kwa helikopta hadi katika uwanja wa ndege mwendo wa saa kumi na moja jioni, wengi walidhani angefululiza hadi Nairobi hasa kwa vile ndege yake ilikuwa tayari imeandaliwa kuondoka.
Lakini alipowasili uwanjani humo, rais aliamkuana na Bw Odinga na wakanong’onezana ndiposa akaabiri mojawapo ya magari yaliyokuwa kwenye msafara wake aina ya Toyota V8 lenye nambari za usajili za kiraia na akafuata gari lililokuwa limembeba Bw Odinga kuelekea mjini Kisumu bila msafara wake wa kawaida wa ulinzi.
Hakukuwa na maafisa wa polisi ambao kawaida anaposafiri huondoa magari mengine barabarani, wala waendesha pikipiki ambao huongoza msafara wake.
Bw Odinga alikuwa amewasili uwanjani dakika chache kabla ya rais kwa helikopta nyingine kwani alikuwa miongoni mwa waliotarajiwa kumlaki na kisha kumuaga akienda Nairobi.
Baada ya kuondoka uwanja wa ndege. msafara wa wawili hao ambao pia ulijumuisha Naibu Gavana wa Kisumu, Mathews Owili na Waziri Raphael Tuju, ulielekea hadi bandari ya Kisumu ambapo siku moja awali, Bw Odinga alikuwa amezindua mpango wa kuondoa mchanga na gugumaji katika Ziwa Victoria.
Baadaye Rais Kenyatta na Bw Odinga walielekea katika mkahawa wa kibinafsi ambapo duru zilisema walikula chakula cha jioni pamoja lakini walichozungumzia kimebaki kuwa siri.
Ni baada ya hapo ambapo waliandamana na ulinzi wao wa maafisa wachache hadi katika uwanja wa ndege na wakawasili dakika chache baada ya saa mbili unusu.
Wakati huu rais hakwenda katika chumba cha wageni mashuhuri uwanjani humo bali alizungumza kwa dakika chache na Bw Odinga na viongozi wengine wa serikali kabla ya kuabiri ndege na kuondoka.
Ndege zingine zilizotarajiwa kuondoka katika uwanja huo zilicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa ndege ya rais, ambayo ilikuwa imepangiwa kuondoka mapema. Rais alitoka katika uwanja wa ndege wa Kisumu saa tatu kasorobo usiku.
Tangu wawili hao walipoweka mwafaka wa maelewano Machi 9 mwaka uliopita, wameendelea kuonyesha urafiki wa ajabu kwa kiasi cha kutia wasiwasi wafuasi wa Naibu Rais William Ruto, wanaoamini Bw Odinga anatumia mwafaka huo kwa manufaa yake ya kibinafsi.
Jana, Bw Muhoho Kenyatta, ambaye ni ndugu mdogo wa Rais Kenyatta, alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria kumbukumbu za miaka 25 tangu kufariki kwa aliyekuwa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga aliyeaga januari 20, 1994. Hafla hiyo ilifanywa Bondo, Kaunti ya Siaya na pia Bw Tuju alikuwepo.
“Wengi wenu hawanifahamu kwa sababu mimi si mwanasiasa bali ni mfanyabiashara na huonekana tu mara moja moja hadharani. Ni mara yangu ya kwanza kufika hapa lakini nitarudi,” akasema Bw Muhoho, ambaye husemekana kuwa mmoja wa wandani wakubwa wa rais.