Habari

Uhuru awapa Wapwani Krisimasi ya mapema

December 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

KALUME KAZUNGU na PSCU

WAKAZI wa Pwani Alhamisi wamepata zawadi ya mapema ya Krismasi kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyezindua miradi kadhaa ya maendeleo eneo hilo.

Kifurushi cha kwanza kilitolewa Kaunti ya Lamu ambapo Rais Kenyatta na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed walikagua ujenzi unaoendelea wa mradi wa Bandari ya Lamu (LAPSSET).

Kufikia sasa, kiegesho cha kwanza cha mradi huo kimekamilika ilhali viegesho vingine viwili vinatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka ujao.

Mradi huo tayari umeleta manufaa tele wakazi wa Lamu na Pwani kwa jumla kwani vijana zaidi ya 2,000 wameajiriwa.

Alipoondoka Lamu, Rais Kenyatta alielekea Mombasa ambako alifungua kiwanda cha kutengeneza magari cha Associated Vehicle Assemblers (AVA) eneo la Miritini.

Mradi wa pili ni ujenzi wa Daraja la Makupa litakalogharimu Sh4.5 bilioni na linalotarajiwa kukamilika Januari 2022.

“Daraja hili litakalokuwa na barabara nne juu ya bahari litachukua nafasi ya barabara ya sasa ya Makupa Causeway iliyojengwa 1929,” ilisema taarifa ya Kitengo cha Habari za Rais (PSCU).

Rais pia alizindua daraja la kuvuka baharini la kutumiwa na watembeaji katika eneo la Liwatoni, ambalo linatarajiwa kufunguliwa Januari 1, 2021. Daraja hilo linatarajiwa kupunguza msongamano kwenye kivuko cha feri cha Likoni.

“Kila siku zaidi ya wananchi 300,000 wanateseka wakienda kazini, hospitali na shughuli zao kwa sababu ya feri. Ndiyo maana nikaona tufanyie wananchi haki kwa kujenga daraja hili litakalowawezesha kutembea bila wasiwasi wa kwenda kungoja feri ama kupanga foleni muda wa saa mbili au muda wa saa tatu na kuchelewa kazini wakisubiri feri,” akasema Rais Kenyatta.

Gavana Hassan Joho wa Mombasa alitaja kuwa kukamilika kwa kivuko cha Liwatoni kutakuwa ni afueni kubwa kwa wananchi ambao kwa sasa wanalazimika kuhatarisha maisha yao wakisongamana kuvuka kwa kutumia feri ambazo ni chache.

“Daraja hili litapunguza msongamano kwenye kivuko cha Likoni, hivyo kupungumza msambao wa Covid-19,” akasema Bw Joho.